Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameeleza kuwa vyomba vya usalama vya Mkoa vimeanza kufanyiakazi habari za uwepo wa mtandao wa matajiri (mapapa) wanaofadhili uvamizi na wizi wa mara kwa mara wa madini katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.
Mheshimiwa Hapi ameeleza hayo leo tarehe 20 Julai, 2022 wakati wa ziara yake katika mgodi huo iliyolenga kupokea taarifa na kujionea maendeleo ya mgodi, kupokea taarifa za zoezi la tathmini ya maeneo yatakayochukuliwa na mgodi kwa ajili ya upanuzi wa shughuli zake na kutoa mrejesho wa maamuzi ya serikali kuhusiana na suala la CSR inayotolewa na mgodi huo.
“Sisi kama Mkoa tumepata taarifa kuwa kuna mtandao wa mapapa (matajiri) ambao unapanga na kuratibu vijana wanaofanya uvamizi na wizi wa mawe yenye madini katika mgodi huo, tunajiandaa kuwashughulikia mapapa wote” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amemuagiza Afisa Madini Mkoa wa Mara Mhandisi Joseph Kumburu, kuangalia sheria za madini na kuushauri Mkoa namna bora ya kuchukua hatua kwa wananchi ambao nyumba zao zipo kwenye mpango wa fidia na hawataki kuchukua fidia lakini nyumba hizo zinatumika na wezi kuvamia mgodi huo.
“Lengo letu ni kuvunja mtandao wa mapapa wanaopanga, kuratibu na kufadhili wizi wa mawe yenye madini katika Mgodi huu ili kulinda mgodi huu ambao serikali pia ina hisa zake mbali ya kupata kodi, mrahabaha, ushuru wa huduma, CSR na manufaa mengine” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa matajiri hao wamekuwa wakifadhili pia tegesha kwa wanajenga nyumba na kupanda miti na mazao ambayo sio halisia katika maeneo ambayo mgodi unataka kupanua uwekezaji wake ili kukwamisha maendeleo ya mgodi huo kwa kutaka walipwe fedha zaidi ya wanazostahili.
“Huku kwenye tegesha tumeshafanya kazi kubwa na kufanikisha wengi wa waliotegesha kukosa fedha walizotarajia kuzipata baada ya kutegesha, wengine ndio hao hao wanaofadhili wavamizi, tutapambana nao” alisema Mheshimiwa Hapi.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Hapi ameutaka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kuwekeza zaidi kwenye teknolojia ya kamera za usalama katika mgodi huo ili kuweza kuwatambua wezi wanaoingia katika mgodi huo kiurahisi.
“Kamera zilizopo sasa hazionyeshi picha vizuri hususan kama wavamizi wameingia wakati wa mvua na mara nyingi uvamizi hutokea zaidi wakati wa mvua kwa sababu wanaoingia mgodini kuiba wanaweza kuona kiurahisi mawe yenye madini” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameuagiza Mgodi huo kuangalia upya suala zima la usalama wa mgodi na haki za binadamu ambapo mgodi umewakataza walinzi wake na askari polisi wanaolinda kutumia silaha wakati wavamizi wanakuja kwa makundi ya watu 50-80 na wanakuwa na mishale, mapanga, marungu na mikuki na wamekuwa wakiwajeruhi askari wanapojaribu kuwazuia.
“Hili lisipofanyiwa kazi mapema askari ndio wanaoumizwa na wavamizi bila ya kupewa uwezo wa kujitetea kwa sababu za haki za binadamu, lakini askari nao ni binadamu pia haki zao pia ziangaliwe na wanapoumia wakiwa kazini mgodi uwasaidie” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amewataka wazabuni wote waliopata zabuni katika mgodi huo kulipa Ushuru wa Huduma (Service Levy) na kuwa na mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa mujibu wa Sheria.
Amemuagiza Meneja Mkuu wa Mgodi huo Bwana Apolinary Lyambiko, kuwasilisha majina ya kampuni zilizopata zabuni, thamani ya mikataba yao na shughuli wanazofanya katika mgodi huo ili waweze kulipa ushuru wa huduma kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mheshimiwa Juma Chikoka ameutaka mgodi kuliwekea mkazo suala la ulinzi wa mgodi na watumishi waliopo mgodini dhidi ya wavamizi wa mgodi huo.
“Kwa hatua zinazochukuliwa sasa, kuna wavutia wavamizi zaidi kuvamia mgodi kwa sababu wanajua wakivamia hamna watakachofanywa na walinzi au askari wa mgodi huo kwa kuwa mgodi hauruhusu askari kutumia silaha, wanaweza kuuteka mgodi huu na kuleta hasara kubwa kwa mwekezaji na kwa Serikali ” ameeleza Mheshimiwa Chikoka.
Mheshimiwa Chikoka ameeleza kuwa pamoja na uwekezaji wa kujenga ukuta na kuweka umeme na nyaya za miba bado wezi hao wanaingia mara kwa mara jambo ambalo ni hatari sana kuachwa liendelee kutokea.
Kwa upande wake, Mthamini kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bwana Rashid Magetha ameeleza kuwa kwa sasa kazi ya uthamini katika vijiji vya Komorera, Genkuru na Kewanja umekamilika na wananchi wameanza kulipwa fidia.
Bwana Magetha ameeleza kuwa kuna wananchi 1808 waliovamia shamba la marehemu Juma Ryoba ambalo linasimamiwa na mtoto wake George Richard Ryoba suala lao lipo mahakamani lakini tayari wameshatengewa fidia yao.
Aidha, Bwana Magetha ameeleza kuwa kuna baadhi ya wananchi wanaogoma kuchukua fidia zao baada ya kutegesha na kutegemea kupata fedha nyingi na matokeo yake kupata fedha kiasi ambacho hawakukitegemea.
“Kuna wananchi 5276 waliotegesha mali zao na maamuzi ya serikali ni kuwa wote waliotegesha wasilipwe fidia, hawa wamekuwa wakizunguka kwa wanasiasa, wanaharakati ili waweze kulipwa fedha na mgodi” alisema Bwana Magetha.
Aidha, Bwana Magetha ameshauri wananchi walipwe fidia na serikali badala ya mfumo wa sasa mgodi ndio unawalipa fidia na kusababisha wananchi mara kwa mara kudai nyongeza ya fidia hizo baada ya kuchukua fidia za awali.
Kwa upande wake Afisa Madini wa Mkoa wa Mara Mhandisi Joseph Kumburu ameeleza kuwa changamoto kubwa iliyopo katika mgodi huo ni uvamizi wa wezi ambao unatokea mara kwa mara.
“Tunayo majina ya wanaotuhumiwa kuwafadhili wezi hao na tumeanza kushirikiana na vyombo vya usalama ili kufanya upelelezi na ikithibitika wachukuliwe hatua” alisema Mhandisi Kimburu.
Aidha, Bwana Kimburu ameeleza kuwa katika mgodi huo kuna uvujaji mkubwa wa siri kwa watumishi wa mgodi, watumishi wa makampuni yanayofanyakazi na mgodi na watumishi wa serikali katika nafasi mbalimbali na tayari wameshaanza kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa