Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameeleza kuwa Mkoa wa Mara utachukua hatua za maksudi kuhakikisha Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Sayansi na Teknolojia kinaanza kudahili wanafunzi mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Hapi ameeleza hayo katika ziara yake aliyoifanya leo tarehe 19 Julai 2021 katika Chuo hicho kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Chuo hicho.
“Kuanza kwa Chuo hiki na hii idadi ya wanafunzi inayotegemewa inaweza kubadilisha kabisa maendeleo ya Mkoa wa Mara ndani ya muda mfupi kwani vyuo vikuu vimekuwa kama kichocheo cha uchumi katika mahali vilipo” ameeleza Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameahidi kuandaa safari maalum pamoja na viongozi wa chuo ili kwenda kumuona Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kufuatilia suala la uanzishaji wa Chuo hiki.
“Mkoa utapambana, kuhakikisha ya kwamba tunawasemea na tunakipigania hiki Chuo kiweze kuanza kwa haraka ili manufaa yaliyotegemewa kutokana na Chuo hiki yaweze kupatikana kwa haraka” amesema Mheshimiwa Hapi.
Ameeleza kuwa Chuo hiki kikikamilika kitakuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi wa Mkoa wa Mara na wananchi wake na kutoa mfano wa Jiji la Mwanza ambapo kabla ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Jiji hilo lilikuwa na uchumi wa kawaida na baada ya kuanza kwa Chuo hicho uchumi wa Mwanza ulipanda sana.
Amewapongeza kwa kufanya kazi ya kuanzisha Chuo na kueleza kuwa kazi hiyo ni ngumu na Chuo kimekaa muda mrefu bila kudahili wanafanzi na kupata viongozi wa Chuo.
Ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika hosteli za wanafunzi ili kuchangamkia fursa hiyo na kuandaa makazi ya wanachuo watakapokuwa wanaanza masomo.
Miradi ambayo ipo katika Chuo hicho ni pamoja na mradi wa ujenzi wa jengo la uchapishaji (University Printing Press) ambao umefadhiliwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambao umeshajengwa na jengo hilo litatumika kama jengo la utawala kwa kuanzia; mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kufundishia utakaofadhiliwa na Benki ya Dunia wa shilingi 103 ambao unategewa kuanza Oktoba 2021; mradi wa ukarabati wa Sekondari ya Oswald Mwang’ombe utakaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5 na mradi Serikali ya Poland wenye gharama ya shilingi bilioni 183 ambao andiko lake limeshawasilishwa.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Lesakit S. B. Mellau ameeleza kuwa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kilianzishwa mwaka 2010 kilikuwa kinaitwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Butiama yaani Butiama University of Agriculture and Allied Sciences lakini baadaye jina la chuo lilibadilika kuakisi nia ya kuanzisha Chuo cha kilimo kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Ili kutekeleza adhma hiyo Serikali ya Mkoa wa Mara Mwaka 2013 kupitia Kamati ya Ushauri wa Mkoa (RCC) iliamua kuwa Chuo Kikuu kijengwe Mkoa wa Mara na kutoa maeneo ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo hiki” alisema Prof. Mellau.
Prof. Mellau ameeleza kuwa Mkoa uliamua kuwa eneo lililokuwa la Kituo cha Uhimilishaji wa Mifugo cha Butiama yaani Butiama Artificial Insemination Center (BAIC) lenye ukubwa wa ekari 573.5 ambalo awali lilijengwa na Cuba kutokana na urafiki wa Hayati Fidel Castro na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kukabidhiwa Wizara ya Kilimo.
Ameyataja maeneo mengine kuwa ni Ikolokonyo lenye ukubwa wa ekari 179 na eneo la Nyambaghembe lenye ukubwa wa ekari 760 katika wilaya ya Butiama; eneo la Kinesi katika Wilaya ya Rorya lenye ukubwa wa ekari 95; na eneo la Kisangula katika Wilaya ya Serengeti lenye ukubwa wa ekari 136; katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo katika Manispaa ya Musoma kuna makubaliano ambayo yanaendelea kuzungumzwa kuwa Chuo kitapewa eneo la kujenga chuo ndani ya eneo la hospitali hiyo kwa ajili ya program za afya.
Prof. Mellau ameeleza kuwa wakati Chuo hicho kinaanza aliyekuwa Mbunge wa Butiama Mheshimiwa Nimrod Mkono alijitolea iliyokuwa Sekondari yake ya Oswald Mwang’ombe kuwa Kampasi anzilishi ya chuo hicho.
Kwa mujibu wa Prof. Mellau mpaka sasa Chuo hicho hakina usajiri wa kudumu na viongozi wa chuo hawajateuliwa ikiwemo Mkuu wa Chuo, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo, Baraza la Chuo pamoja na kamati nyingine za Baraza la Chuo na kwa sasa Chuo kinaendeshwa na Kamati ya Menejimenti ya Chuo pekeyake kikiongozwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma (DVC A) ambaye pia ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo.
Ameeleza kuwa kutokana na hali hiyo Chuo hiki hakiruhusiwa na Kamisheni ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) kudahili wanafunzi, kazi kubwa wanayoifanya kwa sasa ni kutunga hati idhini, miongozo, mitaala na sheria za uendeshaji wa chuo hicho.
Aidha kwa upande wa watumishi ameeleza kuwa Chuo kinawatumishi 79 na kati yao watatu ni wa ngazi za uprofesa wakati wahadhiri wengine wote waliobakia wapo katika ngazi ya Wahadhiri Wasaidizi.
Ameuomba Mkoa ardhi zaidi kwa ajili ya upanuzi wa Chuo hicho kutokana na mahitaji ya ardhi kwa Chuo cha kilimo ni kubwa zaidi lakini ardhi iliyopo kwa sasa inaweza isitoshe kwa siku za usoni.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa