Mkoa wa Mara umeazimia kuongeza ufaulu wa wanafunzi kwa shule zote katika mitihani wa Kidato cha Sita utakaofanyika kitaifa Mwezi Mei, 2022 hapa nchini.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa Bwana Dominicus Lusasi ameeleza hayo wakati akifungua kikao cha tathmini cha kujadili matokeo ya mtihani wa utimilifu kwa Kidato cha Sita mwaka 2022 kilichofanyika katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma.
“Tunataka Mkoa wa Mara uwe wa kwanza katika matokeo ya mtihani wa Kidato cha Sita kitaifa, na ikiwezekana wanafunzi bora katika matokeo hayo watoke katika Mkoa wa Mara” alisema Bwana Lusasi.
Bwana Lusasi ameeleza kuwa pamoja na Mkoa kufanya vizuri katika mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2021, anaamini Mkoa unaweza kufanya vizuri zaidi mwaka huu katika mtihani huo.
Bwana Lusasi amewaagiza Maafisa Elimu wa Halmashauri na Wakuu wa Shule za Sekondari kutumia muda uliobakia katika kuboresha ufundishaji na maandalizi ya wanafunzi kwa ajili ya mtihani wa Taifa.
Aidha amewataka wasimamizi wa elimu kuwasimamia vyema walimu wanaowafundisha wanafunzi ili kufanya maandalizi mazuri ya mitihani mbalimbali ya kitaifa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi – Elimu Bwana Benjamin Oganga amewapongeza walimu kwa kutimiza majukumu yao vizuri hata hivyo amewataka kuongeza juhudi katika kufundisha ili kuondoa daraja sifuri kwa wanafunzi.
“Hawa wanafunzi wamefaulu kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne, kupata daraja sifuri kwenye mitihani yao kunawaharibia maisha yao na wengi wao wanaishia kwenda kutumia vyeti vya kidato cha nne” alisema Bwana Oganga
Bwana Oganga amewataka Wakuu wa Shule za Sekondari kuongeza juhudi katika kusimamia taaluma na kuongeza ufaulu wa wanafunzi wao katika mitihani.
Akitoa taarifa ya matokeo ya mtihani wa utimilifu, Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mara Bwana Ahidi Jailosi Sinene ameeleza kuwa kwa wastani ufaulu wa wanafunzi ni mzuri na umeongezeka ukilinganisha na mtihani wa utimilifu wa mwaka 2021.
Ameeleza kuwa kati ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo, wanafunzi 183 wamepata daraja la kwanza, 1219 wamepata daraja la pili, 1040 wamepata daraja la tatu, 80 wamepata daraja la nne wakati wanafunzi 21 wakipata daraja sifuri.
Bwana Sinene ameeleza kuwa katika ufaulu wa wanafunzi masomo ya sayansi yamefanya vizuri zaidi kuliko masomo ya Sanaa katika mtihani huo uliofanyika kuanzia tarehe 21 Februari, 2022 hadi tarehe 2 Machi, 2022 na kuzihusisha shule zote 26 zenye wanafunzi wa Kidato cha Sita katika Mkoa wa Mara.
Aidha Bwana Sinene ameeleza kuwa Mkoa una wanafunzi 2,586 ambao walitegemewa kufanya mtihani huo hata hivyo wanafunzi 2,543 walifanya mtihani huo huku wanafunzi 46 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali.
Bwana Sinene amezitaja shule zilizofanya vizuri kuwa ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Mkono, iliyoshika nafasi ya kwanza, Shule ya Sekondari ya J. K. Nyerere nafasi ya pili, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe nafasi ya tatu, Shule ya Sekondari ya Natta nafasi ya nne wakati Shule ya Sekondari ya Chief Ihunyo ikiwa imeshika nafasi ya tano.
Aidha amezitaja shule zilizofanya vibaya kimkoa ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Manga ambayo imeshika nafasi ya 26, Shule ya Sekondari ya Ikizu nafasi ya 25 na Musoma Utalii iliyoshika nafasi ya 24.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa