Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri mbalimbali Mkoani Mara kusimamia kikamilifu zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali mkoani humo.
Akizungumza katika kikao cha kugawa awamu ya pili ya vitambulisho vya wajasiriamali kwa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa amewataka viongozi hao kuhakikisha kuwa Mkoa unakuwa na ugawaji wa vitambulisho wa asilimia zaidi ya tisini.
“Sasa kila wilaya ya kila Halmashauri ihakikishe kuwa inagawa vitambulisho kwa zaidi ya asilimia 90 hadi mwisho wa zoezi hili, na atakayeshindwa atajieleza kwa nini imeshindikana” alisema Malima.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa katika awamu ya kwanza kwa mwaka huu wa 2020, Mkoa ulifanikiwa kugawa wastani wa asilimia 62 ya vitambulisho vyote na kuwa Mkoa wa 21 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Malima alieleza kuwa hali hiyoilitokana na baadhi ya halmashauri kufanya vibaya sana na kupata chini ya asilimia 50 katika zoezi hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mheshimiwa Anarose Nyamubi ameeleza kuwa zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara lifanywe na idara zote katika Halmashauri ili kuleta ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Nyamubi ameeleza kuwa kila idara inafanyakazi na watu ambapo baadhi yao ni wafanyabiashara ambao wanahitaji vitambulisho vya wajasiriamali.
“Watendaji wa halmashauri nyingi hawakulipokea suala la vitambulisho vya wajasiriamali vizuri na wamekuwa hawana mwamko wa kulifanyia kazi kama inavyotakiwa” alisema Mheshimiwa Nyamubi.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara Bwana Wallace Mnkando ameeleza kuwa katika awamu hii, vitambulisho vimeletwa kwa namba kwa kutumia mfumo maalum ambao utaiwezesha serikali kufuatilia zoezi la kugawa vitambulisho hivi katika kila hatua.
“Serikali kwa wakati wowote itakuwa na uwezo wa kufuatilia vitambulisho hivi sehemu vilipokwama hatua kwa hatua” alisema Bwana Mnkando.
Katika awamu hii ya pili Mkoa wa Mara umepata vitambulisho 6,000 vitakavyogawiwa katika wilaya za Rorya, Tarime, Musoma, Butiama, Serengeti na Bunda katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa