Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo amefanya ziara yake kwa kwanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na kuahidi kuisadia wilaya ya Rorya kufuatilia ukamilishaji wa barabara ya Mika -Kilongwe yenye kilomita 57 inayojengwa kwa mita 200 hadi 400 kwa mwaka.
Akizungumza katika Ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Rorya Mhe. Mtambi ameeleza kuwa kutokana na umuhimu wa barabara hiyo kwa uchumi wa Wilaya ya Rorya na Mkoa wa Mara kwa ujumla ataifuatilia kuhakikisha inakamilishwa kwa haraka ili barabara hiyo iweze kukamilishwa kwa haraka.
“Nitaifuatilia barabara hii Wizarani ili kuhakikisha inapangiwa bajeti ya kutosha na mkandarasi analipwa kwa wakati ili barabara hii iweze kukamilika kwa wakati” amesema Mhe. Mtambi.
Akizungumzia barabara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Rorya Mhe. Juma Chikoka ameeleza kuwa barabara hiyo ni muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi ya Wilaya ya Rorya hivyo Wilaya inatamani ikamilishwe kwa haraka ili wananchi wapate huduma.
Mhe. Chikoka ameeleza kuwa tayari barabara hiyo imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) hata hivyo imekuwa ikikamilishwa kwa vipande vidogo vidogo sana kila mwaka.
Akiwa katika ofisi za CCM, Mhe. Mtambi amepokelewa na kuzungumza na viongozi na watumishi wa CCM Wilaya ya Rorya wakiongozwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Rorya Bwana Michael Bundala na viongozi wengine.
Baada ya mazungumzo na viongozi wa CCM, Mkuu wa Mkoa amekagua ujenzi wa barabara ya Mika- Kilongwe, ametembelea ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rorya, amezungumza na watumishi wa Halmashauri ya Rorya katika Ukumbi wa Halmashauri na kukagua ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Rorya.
Baada ya hapo Mhe. Mtambi amekagua mradi wa ujenzi wa majengo ya Taasisi ya Utafiti wa Samaki (TAFIRI) katika eneo la Sota na kuhitimisha ziara yake kwa kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya sota.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mtambi ameambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Rorya, viongozi wa CCM Wilaya ya Rorya, Mwenyekiti, Menejimenti na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na watendaji wakuu wa taasisi za umma zilizopo katika wilaya hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa