MARA KUBORESHA USAFI WA MAZINGIRA
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi kesho tarehe 4 Septemba 2021 atazindua Kampeni ya Usafi wa Mazingira kwa Mkoa wa Mara kwa kufanya usafi katika Soko Kuu la Musoma lililopo katika Manispaa ya Musoma kuanzia saa moja asubuhi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kampeni hii ni endelevu na inalengo la kuungarisha Mkoa wa Mara na itafanyika katika kila nyumba, mtaa, vijiji, kata, tarafa, halmashauri na wilaya zote za Mkoa wa Mara.
“Tumejipanga kuhakikisha Mkoa wetu unaondokana na magonjwa yanayotokana na uchafu ambayo yanawaathiri wananchi wetu kwa kusimamia usafi wa mazingira yanayotuzunguka” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa taifa linatumia fedha nyingi kukabiliana na changamoto za kiafya zinazotokana na uchafu na kuwataka viongozi na wataalamu wanaohusika kusimamia usafi katika maeneo yao.
“Tunampango wa kuanzisha mashindano ya usafi hususan katika ngazi ya wilaya na halmashauri zote za Mkoa wa Mara ili kupata halmashauri au wilaya safi na chafu zaidi na baadaye tutakuja kupata nyumba safi zaidi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amewaagiza Maafisa Afya wote wa Mkoa wa Mara kusimamia usafi kwenye mazingira yao na kusimamia sheria, taratibu na miungozo ya usafi na utunzaji wa mazingira.
Uzinduzi wa Kampeni ya afya katika Mkoa wa Mara utahudhuriwa na watumishi wote wa umma, vyombo vya ulinzi na usalama, wananchi na wataalamu wa afya na utafanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya zote sita za Mkoa wa Mara.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma inaonyesha kuwa Katika Manispaa ya Musoma usafi utafanyika katika kata zote za manispaa hiyo kuanzia saa moja asubuhi.
Katika Kata ya Kitaji usafi utafanyika katika eneo la Soko Kuu mjini, Stendi ya zamani, barabara ya Nyerere na Bustani ya Malkia; katika Kata ya Mushikamano usafi utafanyika katika Soko la Saanane, Barabara ya Samia S. H., Barabara ya Kwangwa na eneo la maduka saba; katika Kata ya Mukendo safi utafanyika katika barabara ya Mukendo, maeneo ya Kituo Kikuu cha Polisi, Shule ya Msingi John Bosco na eneo la TRA.
Katika Kata ya Mwigobero usafi utafanyika mwaloni, kivukoni na barabara ya Mwigobero; katika Kata ya Iringo usafi utafanyika katika Mtaro wa Kemondo, Barabara ya Mukendo na Muendo Kati; katika Kata ya Nyasho usafi utafanyika katika soko la Nyasho, Standi ya Nyasho na eneo la Mlango Mmoja.
Katika Kata ya Nyakato usafi utafanyika Musoma basi, barabara za makaburini, Nyerere na Baruti Sekondari, Shule ya Msingi Nyakato, eneo la SIDO na Maziwa; katika Kata ya Bweri usafi utafanyika katika maeneo ya Kariakoo, Stendi ya Bweri, Bweri Centre; na katika Kata ya Rwamlimi ni katika maeneo ya machinjioni na mwalo wa Narusulya.
Aidha katika kata ya Kamnyonge usafi utafanyika katika maeneo ya Majita Road, FFU na Uwanja wa Karume; katika kata ya Nyamatare usafi utafanyika katika soko la Nyamatare wakati katika Kata ya Makoko usafi utafanyika katika mwalo wa Makoko Ziwani.
Ili kufanikisha Kampeni ya Usafi itakayozinduliwa, wananchi wote mnaombwa kushiriki usafi maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya kuzunguka nyumba za kuishi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa