Mkuu wa Mkoa wa Mara amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kuanzisha daftari maalum la wataalamu wa Uhandisi litakalowekwa katika miradi yote ya ujenzi na ukarabati katika Halmashauri zao ili kurahisisha uwajibikaji wa wahandisi katika utekelezaji wa miradi.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 12 Julai, 2022 kwa nyakati tofauti wakati akihudhuria vikao vya mabaraza ya madiwani katika Halmashauri za Wilaya ya Musoma na Manispaa ya Musoma.
“Ninataka kuwepo na madaftari maalum ambayo wahandisi watayatumia kutoa maelekezo kwa mafundi na wasimamizi wengine wa miradi na kutoa maoni yao ili kurahisisha uwajibikaji wa wahandisi katika miradi ya maendeleo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa amebaini katika baadhi ya miradi ya ujenzi wahandisi hawaitembelei mpaka viongozi wanapoenda kuitembelea na baada ya hapo hawarudi tena kurekebisha mapungufu waliyoelekezwa kuyarekebisha.
“Sasa tunataka mhandisi aidhinishe kila hatua ya mradi kwa maandishi na atoe maelekezo yake yote kuhusiana na mradi kwa maandishi ili kiongozi yoyote akifika katika mradi huo aweze kuyaona ili kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi amewataka Wakuu wa Wilaya na Madiwani kuhakikisha kuwa wahandisi wanasimamia miradi ya ujenzi kwa kukagua madaftari ya miradi na kuchukua hatua kwa wahandisi kwa kukwamisha miradi au hasara itakayotokana na utekelezaji mbovu wa mradi husika.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa anaamini madaftari hayo yakisimamiwa vizuri yataimarisha uwajibikaji wa wahandisi, kuboresha usimamizi wa miradi na kupunguza hoja za CAG na mbio za Mwenge wa Uhuru.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kuanzia sasa, kila atakapotembelea mradi atataka kuona madaftari hayo pamoja na maoni au maelekezo yaliyotolewa na wahandisi katika usimamizi wa miradi ya ujenzi na ukarabati katika Mkoa wa Mara.
Maagizo hayo yametolewa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kutembelea Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kuhudhuria vikao vya mabaraza ya madiwani kwa ajili ya kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyoanza leo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa