Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Khalfani Haule leo tarehe 31 Mei, 2023 amefungua kikao cha Afya ya Msingi (PHC) na maandalizi ya mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto katika Mkoa wa Mara katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Haule ameeleza kuwa katika utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa mwaka jana Mkoa wa Mara haukufanya vizuri na sehemu moja wapo ni kiashiria cha utoaji wa matone ya vitamin A na ameshukuru sana uwepo wa wafadhili na mashirika yasiyo ya kiserikali katika eneo hili.
“Ninawataka Wakuu wa Wilaya wote kusimamia vizuri zoezi hili na kuzindua zoezi la utoaji wa matone ya Vitamin A katika maeneo yenu na kuwahusisha viongozi wa maeneo husika wote katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa” amesema Dkt. Haule.
Mheshimiwa Haule ameeleza kuwa utoaji wa matone ya vitamin A ambayo ni muhimu sana katika kinga ya mwili, kuzuia upofu na magonjwa mengine.
Aidha, Dkt. Haule amezitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kutoa kipaumbele cha kuboresha afya ya watoto kwa kusimamia na kutekeleza kikamilifu mkataba wa lishe.
Mwakilishi huyo wa Mkuu wa Mkoa ameishukuru Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kuendelea kutoa wataalamu na wadau wote wa afya waliohusika na masuala ya lishe na utoaji wa matone ya Vitamin A kwa kufadhili kikao hicho.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Zabron Masatu ameeleza kuwa mpango wa Mkoa wa Mara kwa mwaka huu ni kuwa kinara katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe.
Dkt. Masatu ameeleza kuwa utoaji wa chanjo ya matone ya vitamin A kwa watoto chini ya miaka mitano upo katika viashiria muhimu vya utekelezaji wa mkataba wa lishe hapa nchini.
“Mkoa wa Mara unatarajia kuanza kampeni ya utoaji wa Vitamin A kuanzia tarehe 01-30 Juni, 2023 kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano” alisema Dkt. Masatu.
Dkt. Masatu ameeleza kuwa utoaji wa matone ya Vitamin A hufanyika mara mbili kila mwaka katika miezi ya Juni na Desemba na masuala mbalimbali ikiwemo utoaji wa Vitamin A, utambuzi wa
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Peter Kaswahili ameeleza kuwa anaamini maandalizi ya usambazaji wa vitamin A na uhamasishaji katika Mkoa wa Mara umeshafanyika ili kuruhusu zoezi hilo kuanza.
Dkt. Kaswahili amewataka watumishi wa sekta ya afya watakaohusika na zoezi hilo kujaza taarifa inavyotakiwa katika mfumo ili kuweza kuboresha takwimu za masuala ya lishe katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Helen Keller International Dkt. Deogratius Damas Ngome ameeleza kuwa shirika hilo limejikita katika magonjwa ya macho, masuala ya lishe na magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele.
Dkt. Ngome ameeleza kuwa Mkoa wa Mara ni miungoni mwa mikoa 14 ambayo ilikuwa haina msaada wa wadau katika kutoa matone ya vitamin A; Mkoa una wakazi wengi kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022 na kutokana na mahusiano yaliyopo anaamini wanaweza kufanya kazi vizuri zaidi wakiwa katika Mkoa wa Mara.
Kikao cha Afya ya Msingi cha maandalizi ya kuanza kwa kampeni ya utoaji wa matone ya vitamin A kimefayika leo tarehe 31 Mei, 2023 katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa