Serikali imeipongeza Mikoa ya Mara na Arusha kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu inayofadhiliwa na mradi wa GPE Lanes II hapa nchini na kuiwezesha Tanzania kuendelea kupata misaada zaidi kutoka kwa wafadhili mbailili ya kuimarisha sekta ya elimu.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara ya siku nne katika mikoa ya Mara na Arusha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi Dkt. Charles Wilson Mahera amesema miradi yote iliyotembelewa imetekelezwa vizuri na viongozi na wasimamizi wa GPE Lanes II wamefurahishwa na miradi hiyo.
“Miradi yote tuliyoitembelea imetekelezwa kwa kiwango na ubora wa miradi hiyo na wafadhili wamefurahishwa zaidi kuona mchango wa jamii na wanufaika katika utekelezaji wa miradi hiyo” amesema Dkt. Mahera.
Dkt. Mahera amewataka viongozi wa Mikoa na Halmashauri kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo kwa viwango na weledi ili kuimarisha miundombinu ya sekta mbalimbali na hususan wakati huu ambapo Serikali imeanza kutekeleza mtaala mpya wa elimu na kutoa fedha za kujenga shule za amali katika mikoa yote hapa nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Msingi na Awali, ambaye katika ziara hiyo amemwakilisha Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bibi Susan Nussu amesema ameridhishwa na miradi yote waliyoitembelea na kupongeza kwa namna wasimamizi na watekelezaji wa miradi hiyo walivyojiongeza.
“Katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma, wanafunzi wanaosoma ufundi wameshiriki kujenga madarasa na kutengeneza samani jambo ambalo limesaidia shule hiyo kujenga pia ofisi ya walimu kwa kutumia fedha zilizolenga kujenga madarasa mawili na matundu sita ya vyoo” amesema Bibi Nussu.
Bibi Nussu amesema katika Shule ya Msingi ya Ibwagalilo awali watoto walikuwa wanaenda mbali kufuata Shule ya Msingi Nyamalebwe ambayo ndio kwa wakati huo ilikuwa jirani kwa watoto hao na utoro wa wanafunzi katika shule hiyo ulikuwa mkubwa na ufaulu haukuwa mzuri kutokana na umbali huo.
“Kwa sasa ufaulu wa wanafunzi wa Ibwagalilo wanafanya vizuri katika masomo yao na matokeo ya upimaji wa darasa la nne kwa mwaka 2022 na 2023 wamefaulu kwa asilimia 100, utoro hamna na wazazi wameitikia wito wa kuchangia chakula cha wanafunzi” amesema Bibi Nussu.
Bibi Nussu amesema katika Shule ya Msingi ya Ibwagalilo iliyojengwa na wafadhili hao hamna mwanafunzi ambaye hajui kusoma, kuhesabu na kuandika jambo ambalo ni mafanikio baada ya wanafunzi kuboreshewa mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na zana za ufundishaji kwa wanafunzi wa awali.
Viongozi hao wametoa pongezi hizo wakati wa kuhitimisha ziara ya siku nne katika mikoa ya mara na Arusha iliyoongozwa na Balozi wa Sweeden nchini Tanzania Mhe. Charlotta Macias Ozaki pamoja na viongozi wengine wanaosimamia mradi wa Global Partnership for Education (GPE) Lanes II.
Wakiwa katika Mkoa wa Mara wageni hao wametembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Manispaa ya Musoma ambapo wamekatembelea Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma na Shule ya Msingi Mwembeni B.
Katika Wilaya ya Butiama, ugenzi huo umetembelea Shule ya Msingi Bisumwa kukagua ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya awali na baadaye kutembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wakiwa hapo walipokelewa na wanafamilia wakiongozwa na Bwana Makongoro Nyerere.
Wageni wengine walioshiriki ziara hiyo ni pamoja na Naibu Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. Olukemi Williams, wasimamizi wa mradi wa GPE Lanes II kutoka Ubalozi wa Sweeden na Uingereza, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa