Uzalishaji katika Mgodi wa Dhahabu wa Irasanilo unaomilikiwa na wachimbaji wadogo umeongezeka kwa sasa wanapata wastani wa zaidi ya kilo moja hadi moja na nusu ya dhahabu kwa mwezi jambo ambalo limeongeza ukusanyaji wa kodi na ushuru wa huduma unaotokana na uchimbaji wa madini.
Hayo yameelezwa leo tarehe 7 Septemba, 2022 na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara Mhandisi Joseph Kumburu wakati akitoa taarifa ya Mgodi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee na kuongeza kuwa kuongezeka kwa uzalishaji huo kumeenda sambamba na udhibiti wa utoroshaji holela wa madini uliokuwa ukifanyika hapo awali.
“Awali uzalishaji katika Mgodi wa Dhahabu wa Irasanilo ulikuwa chini lakini pia kulikuwa na tatizo la utoroshaji wa madini uliokuwa ukifanyika katika Mgodi Huu” alisema Mhandisi Kumburu.
Mhandisi Kumburu ameeleza kuwa baada ya uzalishaji kuongezeka na kudhibiti utoroshaji wa madini katika mgodi huo, kwa sasa mapato ya Serikali Kuu na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama yameongezeka sana.
“Mfano ni makusanyo ya ushuru wa huduma (service Levy) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ambapo awali Halmashauri ilikuwa inakusanya shilingi milioni tano kwa mwaka, lakini baada ya maboresho yaliyofanyika kwa sasa Halmashauri inakusanya zaidi ya milioni tano kwa mwezi” alisema Mhandisi Kumburu.
Mhandisi Kumburu ameeleza kuwa ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ni kubwa na hii ni zaidi ya mara kumi ya ushuru wa huduma ambayo mgodi huo ulikuwa unalipa hapo awali kwa mwaka mzima.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mwal. Moses Kaegele ameeleza kuwa awali Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ilikuwa na mapato kidogo sana yanayotokana na mgodi huo, lakini kwa sasa Mgodi wa Irasanilo umekuwa ni tegemeo la mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Amewataka wachimbaji katika mgodi huo kuendelea kulipa kodi na ushuru kwa Serikali ili kuinua huduma za jamii katika eneo la Buhemba na Wilaya ya Butiama kwa ujumla.
“Tunafahamu kuwa watu wanawarubuni wachimbaji kuacha kutoa kodi na ushuru kwa Serikali, niwaombe tu tuachane kugomea taratibu za kisheria zilizowekwa na Serikali, kwa hilo tutakuwa wakali sana kusimamia mapato ya Serikali” alisema Mheshimiwa Kaegele.
Kwa upande wao, wachimbaji hao pamoja na viongozi wa serikali za vijiji waliokuwepo wameiomba Serikali kuongeza miundombinu ya huduma za jamii ikiwemo shule za msingi na shule za sekondari na Kituo cha Afya.
“Hapa kuna watu wengi sana na kutokana na hilo watoto pia ni wengi sana, shule moja haitoshi zinahitajika shule tatu za msingi na angalau shule mbili za Sekondari katika eneo hili” walisema wachimbaji hao.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, watumishi mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa