Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) leo amefanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Msingi Miembeni, Mji wa Bunda na kuwahakikishia wananchi wa Kata ya Nyatwali kuwa malipo ya fidia yatalipwa wakati wowote kuanzia sasa.
Mhe. Majaliwa ametoa kauli hiyo baada ya wabunge wa Mkoa wa Mara kwa nyakati tofauti kuulizia malipo hayo na kuiomba Serikali kuwalipa wananchi kwa haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za maendeleo katika maeneo mapya.
“Mazoezi ya tathmini ya kina na uhakiki wa tathmini iliyofanyika yamekamilika, kwa sasa wakati wowote wananchi wa Kata ya Nyatwali wanaweza kulipwa fidia zao” amesema Mhe. Majaliwa.
Ameeleza kuwa mpaka sasa Serikali haijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi wa Kata ya Nyatwali kuhusu kupunjwa au baadhi ya mali zao halali kutothaminiwa katika zoezi la awali na hivyo ni matumaini yake kuwa hakutakuwa na mtu analalamika baada ya malipo ya fidia kutolewa kwa wananchi.
Amewapongeza wananchi wa Nyatwali kwa kudai fidia yao kwa amani na utulivu na bila vurugu yoyote jambo ambalo amesema ni mfano wa kuigwa na wananchi wengine wenye migogoro ya fidia kama Nyatwali.
Aidha, akiwa katika Mkutano huo Mhe. Majaliwa ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Mara kwa mapokezi mazuri tangu alipowasili Mkoa wa Mara tarehe 25 Februari, 2024 kuanza ziara yake.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa