Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amewataka watanzania kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ili kujionea urithi mkubwa ambao watanzania tumepewa na mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Malima ameeleza hayo leo tarehe 21 Februari katika eneo la Barafu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti alipoambatana na wahifadhi wa Serengeti na waandishi wa habari kwa ajili ya kujionea tukio la kuzaliana kwa nyumbu ambalo hutokea katika kipindi hiki kila mwaka.
“Serengeti ni urithi mkubwa sana tuliopewa na Mwenyezi Mungu, na watu kutoka mataifa yote wanakuja kuuangalia lakini sisi wenyenayo hatuji sana kama tunavyotarajiwa” alisema Malima.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa Mkoa wa Mara umejipanga kuhamasisha utalii wa ndani ili kutoa fursa kwa wananchi wake na wawekezaji kuwekeza zaidi katika fursa zinazotokana na utalii wa wanyamapori katika hifadhi hiyo.
Ameeleza kuwa Mkoa unajivunia Serengeti kuwa hifadhi bora ya Afrika kwa mwaka wa pili mfululizo jambo ambalo amesema sio la bahati mbaya bali ni utekelezaji wa mkakati madhubuti wa kukuza utalii hapa nchini.
Amewataka watanzania kuhamasisha uhifadhi endelevu kwa manufaa ya vizazi ya sasa na vizazi vijavyo na kuepukana na ujangili ambao unaua wanyama na kuhalibu ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Bwana Masana Mwishawa ameeleza kuwa nyumbu katika hifadhi hiyo huzaliana kwa siku 28 kila mwaka kati ya miezi ya Februari na Machi.
“Wanyama hawa huzaliana katika kipindi hiki kwa wakati mmoja ni mbinu yao ya ulinzi li kuweza kujilinda na wanyama wanaokula nyama ambao ni wengi katika hifadhi hii” alisema Mwishawa.
Bwana Mwishawa ameeleza kuwa inaadiriwa katika kipindi hiki nyumbu zaidi ya 1,600,000 pamoja na pundamilia na wanyama wengine hukusanyika katika maeneo yenye uwanda wa tambarare ambapo nyumbu takriban 5,000 hadi 8,000 huzaliwa kwa siku na katika msimu mzima nyumbu taktriban 500,000 huzaliwa.
Bwana Mwishawa ameeleza tukio la kuzaliana kwa nyumbu ni tukio kubwa ambalo ndilo chanzo cha msafara wa nyumbu ambapo baadaye wanavuka mto Grumeti, na baadaye wanavuka mto Mara kwenda hifadhi ya Masai Mara nchini Kenya na baadaye kurudi Tanzania katika tambarare hizo na kuzaliana.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ina eneo la kilomita za mraba 14,800 ambapo asilimia 70 ya eneo lote la hifadhi ya Serengeti lipo katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa