Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa kutoa elimu zaidi kuhusiana na masuala muhimu ya uchaguzi kwa wasimamizi na wadau wa uchaguzi ili kuimarisha demokrasia hapa nchini.
Mheshimiwa Malima amesema hayo leo tarehe 24 Agosti 2020 ofisini kwake wakati alipowapokea maafisa kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Kanda ya Ziwa Mashariki ambao watasimamia uchaguzi katika Mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga.
“Wasimamizi wa uchaguzi kwa ngazi zote wanahitaji elimu ya sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ili kuimarisha demokrasia yetu hapa Tanzania”. Alisema Mheshimiwa Malima.
Ameeleza kuwa elimu juu ya sheria hizi katika ngazi mbalimbali za usimamizi wa uchaguzi itaongeza uwajibikaji na kuimarisha picha ya demokrasia ya Tanzania kwa wadau wote ambao wangependa kuufuatilia.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa kuna baadhi ya vyama vinajua kabisa havitashinda lakini vitajitahidi kuwekeza katika kuleta chokochoko ili kuvuruga uchaguzi na kuionyesha dunia kuwa uchaguzi wa Tanzania haukuwa wa haki.
Aidha Mheshimiwa Malima amemwagiza Mratibu wa Masuala ya Uchaguzi katika Mkoa wa Mara Bwana Dominick Rusasi kuandaa mafunzo ya sheria za vyama vya siasa na gharama za uchaguzi kwa Makatibu Tarafa na Watendaji wa Kata wa Mkoa wa Mara ili kuimarisha usimamizi wa uchaguzi.
Awali, maafisa kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyamavya siasa waliotoa pendekezo la kutoa mafunzo kuhusiana na sheria hizo kwa wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya majimbo na wasimamizi wa uchaguzi kwa ngazi ya Mkoa.
Maafisa waliojitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara ni Bibi Clevu Sepaku, Msimamizi wa Uchaguzi Kanda ya Ziwa Mashariki ambaye aliambatana na Bwana Mtibora Suleiman na Bwana Frank Shija.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa