Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amewataka wananchi na wadau mbalimbali wa mahakama kuwasilisha malalamiko yanayohusu maadili ya maafisa wa mahakama kwenye kamati ya Mkoa ya kushughulikia malalamiko hayo ili yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu ya sheria.
Mheshimiwa Malima ametoa kauli hiyo leo tarehe 19 Februari 2021 wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na masuala mbalimbali ya maendeleo kwa Mkoa wa Mara.
“Natoa wito kwa wananchi wote wenye malalamiko yanayohusu maadili ya maafisa wa mahakama kuwasilisha malalamiko yao kwa maandishi na kamati yangu itatenda haki ya kusikiliza pande zote mbili zinazohusika kabla ya kutoa mapendekezo kwa Jaji Mfawidhi” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 50 cha Sheria ya Utumishi wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011 kamati ya maadili inaongozwa na yeye kama mwenyekiti wake na wajumbe wengine sita ambao ni pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa ambaye ndiye kaatibu wa kamati hiyo.
Ameeleza kuwa majukumu ya kamati ya maadili wa maafisa wa mahakama ni kuchunguza malalamiko ya ukiukwaji wa maadili dhidi ya mahakimu na wasaidizi wa sheria wa majaji na kufanya maamuzi na kuandaa repoti ya uchunguzi wa malalamiko.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Malima wananchi wanaweza kulalamikia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna kesi ilivyoshughulikiwa; tuhuma za rushwa; kushindwa kutekeleza majukumu na vitendo vinavyokiuka kanuni za maadili ya maafisa wa mahakama.
Aidha amewataka wananchi kutoa malalamiko yao kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara ndani ya miezi sita baada ya tukio kutokea kwa maandishi na kwa lugha ya Kiswahili ili kamati iweze kuyafanyia kazi malalamiko yao.
Mheshimiwa Malima ameahidi kamati hiyo kutenda haki katika kusikiliza na kushughulikia malalamiko yatakayowasilishwa kabla ya kutoa mapendekezo ya kamati kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa