Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amewataka wananchi wa eneo la Nyamongo wanaoishi jirani na mgodi wa Barrick North Mara kujiongeza kwa kuunda vikundi vya uzalishaji mali ili kujiletea maendeleo.
Mheshimiwa Malima alitoa kauli hiyo tarehe 5 Mei 2020 wakati akizungumza na wananchi wa Nyamongo kuhusiana na malipo ya fidia kwenye maeneo yao yatakayochukuliwa na Mgodi wa Barrick North Mara.
“Jipangeni sasa muanzishe vikundi vya uzalishaji mali maeneo yapo na masoko hapa tunayo ya uhakika kama tutazalisha kwa kufuata kanuni za kitaalamu” alisema Malima.
Aliwaambia wananchi kuuona mgodi wa Mgodi wa North Mara kama fursa ambayo Mungu aliiweka hapo na sio kama adau wanaehitaji kugombana nae kila wakati. Amewaahidi pia wakizalisha vitu vizuri ambavyo vinaweza kutumika mgodini yeye atawasaidia kuuomba mgodi ili uweze kununua ili kujikomboa kiuchumi.
“Mkizalisha hapa mayai, maziwa, nyama, vyakula vingine kwa wingi na kwa ubora, hawa (Mgodi wa North Mara) hawatanunua kutoka mbali wakati hapa vipo na sisi kama serikali tutahakikisha mnapata ninyi kwanza” Alisema Malima.
Aliwashauri watakaoanzisha vikundi kama watahitaji mtaji wa kuendeleza uzalishaji wao kuwasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambaye anafedha za kuwezesha vikundi vya vijana, walemavu na wanawake katika shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhandisi Mtemi Msafiri ameeleza kuwa Nyamongo ni eneo linalofaa sana kwa ajili ya uwekezaji mkubwa kwa sababu soko lipo.
“Mkakati wa Wilaya kwa sasa ni kuanzisha shughuli ya kilimo cha mpunga karibu na eneo hili na kuuzalisha kwa wingi ili tuweze kuwaomba wenzetu wa mgodi waununue” alisema Eng. Msafiri.
Eneo la Nyamongo ni eneo linalozunguka Mgodi wa Barrick North Mara ambalo kwa muda mrefu wananchi wake walikuwa wanaruka ukuta na kuingia mgodini kuchukua mabaki ya mchanga katika mgodi huo kitu ambacho kimekuwa kikihatarisha maisha yao.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa