Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amewataka viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kujitathmini na kuwatendea haki wananchi wa halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Malima ametoa kauli hiyo leo tarehe 4 Juni 2020 wakati alipohudhuria baraza maalum la madiwani kwa ajili ya kujadili hoja mbalimbali zilizotolewa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Ninaomba wote tuliopo hapa leo tujitathmini, tunaitendea haki halmashauri hii na kama tunayoyafanya yanawanufaisha wananchi au yanaendana na dhamira ya serikali ya kuiendeleza halmashauri hii ambayo ipo nyumbani kwa Baba wa Taifa?” alisema Malima.
Aidha amewaasa madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Butiama kushirikiana na kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zimejitokeza baina yao.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa ameanza ziara yake katika Halmashauri ya Butiama kwa sababu madiwani na watendaji wa Halmashauri hawakuitendea haki halmashauri hiyo na kuiwezesha kupata hati yenye mashaka katika taarifa ya CAG ya mwaka wa fedha 2018/2019.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Malima, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ingeweza kupata mapato mengi ya ndani kama watendaji na madiwani na viongozi wengine wangeshirikiana na kuwa kitu kimoja.
Katika taarifa ya CAG, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ilikuwa na jumla ya hoja 72 ambapo kati yake hoja 41 ni za zamani kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2017/2018 wakati hoja 31 ni kwa ajili ya mwaka wa fedha 2018/2019.
Hata hivyo baadhi ya hoja hizo za CAG zimefutwa baada ya CAG kuridhika na majibu yaliyotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na nyingine zipo katika hatua mbalimbali wa utekelezaji wake.
Wakizungumza katika kikao hicho madiwani walikiri kuwepo kwa changamoto kubwa za ushirikiano baina ya madiwani na watendaji hususan kwa baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri hiyo waliookuwepo hapo awali. Hata hivyo wamempongeza Mkurugenzi wa sasa Bibi Diana Sound kwa kazi kubwa ambayo ameanza kuifanya katika halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kurejesha vikao vya kawaida vya Baraza la Madiwani.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa