Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amewataka wazazi wa Mkoa wa Mara kuwalinda watoto wao dhidi ya homa ya mapafu inayosababishwa na virusi ya Corona maarufu kama COVID 19.
Mheshimiwa Malima ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa eneo la Nyamongo katika Wilaya ya Tarime kuhusiana na malipo ya fidia ya maeneo yao yatakayochukuliwa na Mgodi wa Barrick North Mara.
“Serikali haijafunga shule na vyuo ili watoto watembee ovyo mitaani na kushiriki shughuli zinazowahatarisha na maambukizi ya Corona, serikali ilitaka wazazi wawalinde watoto wao na ikiwezekana wakae nyumbani” alisema Malima.
Ameeleza kuwa kwa sasa wanafunzi hawapo likizo ya kawaida na wanatakiwa wakae ndani ili waweze kulindwa na sio kuachiwa wanatembea ovyo na kufanyishwa shughuli katika maeneo hatarishi hususan kwenye mikusanyiko ya watu.
Aidha amewapongeza wananchi hao kwa kuchukua tahadhari ya Corona kwa kukaa mbalimbali katika mkutano huo jambo ambalo amesema linauwezo wa kuwaepusha watu na Corona.
Amewataka kutoa taarifa za wageni wanaoingia katika maeneo yao hususan kutoka nchi jirani ya Kenya bila kufuata utaratibu ili waweze kudhibitiwa na hivyo kudhibiti ugonjwa huo kuingia Mkoa wa Mara.
Amewataarifu kuwa kwa sasa shughuli zote za misiba zitafanywa na watu wachache na ndani ya muda mfupi ili kuweza kuwakinga watu dhidi ya maambukizi ya Corona aidha kutakuwa hamna shughuli za sherehe zozote mpaka Corona itakapokuwa haipo tena au itakapokuwa imedhibitiwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhandisi Mtemi Msafiri ameeleza kuwa kwa sasa wamebaini baadhi ya wazazi wanawapeleka watoto wao ambao ni wanafunzi kukeketwa na kuwaozesha katika kipindi hiki.
“Ofisi yangu bado inafuatilia suala hili, na nitoe rai kama jambo hili ni la kweli liachwe mara moja ili kuwalinda watoto waweze kuendelea na masomo yao” alisema Eng. Msafiri.
Mkoa wa Mara kwa sasa una watu waliopo karantini baada ya kusafiri nje ya nchi na hauna mgonjwa aliyethibitika kuwa na Corona baada ya mgonjwa aliyekuwepo kupona na kurudi nyumbani kwake katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Serikali imefunga shule na vyuo vyote kwa muda usiojulikana ili kuweza kuepusha mikusanyiko inayoweza kusababisha maambukizi ya virusi vya Corona kwa wanafunzi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa