Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kujenga vichomea taka vinne kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati za halmashauri hiyo hadi tarehe 30 Juni 2020.
Mheshimiwa Malima ametoa agizo hilo leo tarehe 8 Juni 2020 katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
“Haiwezekani vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika halmashauri hii kutokuwa na vichomea taka na mashimo ya kutupia kondo la nyuma, hali hii haikubaliki” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa amesema kwa kuwa ujenzi wa vichomea taka na mashimo haya vilikuwemo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 anamtaka Mkurugenzi kufanyakazi hiyo katika muda uliobakia na kuwasilisha taarifa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Aidha amemtaka Mkurugenzi huyo kuwasimamia vizuri watendaji wake hususan katika kujibu hoja mbalimbali zinazotolewa na wakaguzi wa hesabu za serikali.
“Mimi nimesikitika sana kwa hoja hizi, ninavyoamini mimi huyu Mkurugenzi ni bora sana lakini watendaji wake mumemwangusha. Na hata ukiangalia hoja nyingi ni ndogondogo sana na zina majibu yake sasa sielewi kwa nini hazikuwasilishwa kwa mkaguzi wakati anakagua” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Mara ameahidi kuandika barua kwa Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu fedha za ujenzi wa Hospitali ya wilaya ambazo zilichukuliwa na Hazina baada ya mwaka wa fedha 2018/2019 kuisha zaidi shilingi milioni 500 ambazo bado zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Naano Anney ameipongeza halmashauri hiyo kwa ukusanyaji wa mapato na kwa mwaka wa fedha 2019/2020 wamefikia asilimia 97 ya lengo la makusanyo.
Aidha Dkt. Anney ameipongeza halmashauri hiyo kwa kuongeza mapato yanayotokana na uvuvi ambapo awali halmashauri ilikuwa inapata shilingi milioni 100 kwa mwaka wakati kwa mwaka huu 2019/2020 halmashauri imekusanya zaidi ya shilingi milioni 800.
Katika ukaguzi wa Mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ilipata hati safi na ilikuwa na jumla hoja 60 ambapo kati ya hizo hoja za nyuma 17 na hoja mpya za mwaka 2018/2019 ni 43.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa