MALIMA AIPONGEZA MUWASA KWA UKAMILISHAJI WA MIRADI KWA WAKATI
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) kwa kukamilisha miradi mikubwa miwili ya maji katika Wilaya ya Serengeti iliyokuwa umekwama kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Malima alitoa pongezi hizo wakati alipokagua miradi ya maji miwili inayotekelezwa na MUWASA katika Wilaya ya Serengeti leo tarehe 4 Machi 2021 ambapo ameridhia miradi hiyo kufunguliwa katika maadhimisho ya Wiki ya Maji inayotarajia kuanza tarehe Machi 16 hadi 22 mwaka huu.
“Ninawapongeza sana kwa utekelezaji mzuri wa miradi hii iliyokwama kwa muda mrefu ambayo sasa ipo mbioni kukamilika na kuwapatia huduma ya maji wananchi wa Mji wa Mugumu na baadhi ya vijiji katika Wilaya ya Serengeti”alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima ameitaka MUWASA kujiamini na kuonyesha uwezo wake katika utekelezaji wa miradi ili waweze kupata miradi mingine ya maji ambayo inasuasua katika Mkoa wa Mara ili wananchi wapate huduma ya maji.
Mheshimiwa Malima ametembelea miradi ya ujenzi wa Chujio la Manchira katika mji wa Mugumu na mradi wa ujenzi wa tanki na usambazaji wa maji katika kijiji cha Kitunguruma ambayo awali ilikuwa ikifanywa na wakandarasi wengine na serikali ilisitisha mikataba yao baada ya kushindwa kutekeleza miradi hiyo kwa wakati na kuipa MUWASA kuimalizia kwa kutumia mfumo wa Force Account.
Aidha Mheshimiwa Malima ameiagiza MUWASA na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Serengeti kuangalia uwezekano wa maji ya mradi wa kijiji cha Kitunguruma kusambazwa katika vijiji jirani ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na miradi hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MUWASA Bibi Joyce Msiru ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa Chujio la Manchira ulianza kutekelezwa Machi 2015 na mkandarasi Pet Coorperation Ltd kwa gharama ya shilingi 2,173,513,900 na mkataba huo ulivunjwa tarehe 8 Januari 2020 baada ya mkandarasi kushindwa kukamilisha kwa wakati.
“Baadaye mradi huu tulikabidhiwa MUWASA kwa gharama ya shilingi 947,744,707.40 kuanzia Oktoba 2020 na ulitegemewa kukamilika mwishoni mwa Machi 2021, kwa sasa mradi huu umefikia asilimia 90 ya utekelezaji” alisema Bibi Msiru.
Aidha katika mradi wa kusambaza maji katika Kijiji cha Kitunguruma Bibi Msiru amesema mradi huu ulikuwa unatekelezwa na mkandarasi Urban and Rural Engineering Services Ltd ya Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi 1, 153, 608,780 kuanzia Juni 4, 2018 na ulipangwa kukamilika Juni 4, 2019.
Hata hivyo mkataba huu ulivunjwa na serikali tarehe 2 Desemba 2020 kutokana na kusuasua kwa utekelezaji wa mradi na baadaye serikali ilikabidhi mradi huo kwa MUWASA Mei 2020 na ulitarajiwa kukamilika Desemba 2020.
Bibi Msiru ameeleza kuwa MUWASA wametekeleza mradi huu kwa gharama za shilingi 748,501,193.06 ikijumlisha kiasi ambacho alilipwa mkandarasi wa awali na hivyo serikali kuokoa shilingi 405,107,586.96 na kwa sasa mradi umekamilika kwa asilimia 95 kinachosubiriwa ni TANESCO kufunga transfoma za umeme ili kuanza kusambaza maji katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Bibi Msiru, miradi hiyo miwili inafadhiliwa na Wizara ya Maji kupitia Mfuko wa Maji.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa