Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameitaka halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuongeza nguvu katika kilimo ili kupanua uwigo wa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Malima ametoa kauli hiyo wakati alipohudhuria kikao maalum cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2020.
“Halmashauri hii inauwezo mkubwa wa kuongeza mapato ya ndani kama itatoa kipaumbele katika kilimo cha mazao ya pamba, kahawa, miwa na mazao mengine” alisema Mheshimiwa Malima.
Alisema halmashauri hiyo ina maeneo mazuri na makubwa sana kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara lakini kilimo hakijajapewa kipaumbele katika uwekezaji na ufuatiliaji.
Mheshimiwa Malima alisema kuwa maeneo mengine yanayohitaji kipaumbele katika halmashauri hiyo ni pamoja na mifugo na misitu.
“Bahati nzuri halmashauri hii imebarikiwa vitu viti sana, mapato yake yalitakwa kuwa makubwa sana ukilinganisha na hali halisi iliyopo sasa” alisema Mheshimiwa Malima.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Malima kutegemea mapato yanayotokana na uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pekee hakuwezi kuiinua halmashauri hiyo na wananchi wake wote kiuchumi.
Aidha amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kuweza kuingia katika halmashauri hiyo. Akatolea mfano wa mwekezaji ambaye amejenga hoteli ya kisasa ambaye anaambiwa abomoe kwa sababu eneo hilo linataka kufanyiwa uwekezaji mwingine.
Wakati huo huo katika kikao hicho aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kisangula kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mheshimiwa Samson Riyoba ametangaza kukihama chama hicho na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti katika ukaguzi wa mwaka wa fedha 2018/2019 ilipata hati safi na ilikuwa na hoja za nyuma 37 na hoja mpya 27.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa