Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu leo tarehe 16 Februari, 2024 amekutana na kufanya kikao na Wakuu wa Shule za Sekondari za Mkoa wa Mara katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma na kuwataka kutimiza wajibu wao kwa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika mkutano huo, Bwana Makungu amesema Wakuu wa Shule kutokana na majukumu yao wananafasi kubwa sana katika maendeleo ya Taifa letu ikiwa ni pamoja na malezi kwa vijana ili kupata Taifa lenye vijana wenye maadili na nidhamu.
“Mnanafasi ya kutengeneza watu wenye uwezo wa kuwaandaa Watanzania kutoa mchango timilifu katika maendeleo ya nchi yao” amesema Bwana Makungu na kongeza kuwa hayo yote yatafanyika ikiwa watatimiza wajibu wao wa malezi, usimamizi wa ufundishaji na nidhamu katika shule hizo.
Aidha, amewataka kuacha kufanyakazi kwa mazoea na kuanzisha makundi yasiyo na tija baina ya walimu na wanafunzi kwani kazi hiyo sio ya kupigiwa kura, ni kazi ya kuteuliwa kutokana na sifa na hivyo wasivunje taratibu kutoa nafasi ya kupendwa na wasiofuata utaratibu.
Bwana Makungu amewataka Wakuu wa Shule wanapokabiliana na changamoto katika usimamizi wa miradi ya maendeleo katika shule zao watoe taarifa na kuomba ushauri kwa wakuu wa shule wengine, viongozi wa Halmashauri, Mkoa hadi Wizara ili kufanikisha malengo ya Serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara amewataka Wakuu wa Shule kusimamia ufundishaji wa wanafunzi ili kuwanusuru wanafunzi kusoma kwa miaka minne na kufeli jambo ambalo linamfanya mwanafunzi huyo asiweze kupata fursa zaidi za kujiendeleza au kuajiriwa kwa baadaye.
Amewataka kusimamia nidhamu na kudhibiti mahusiano yasiyo faa baina ya walimu na wanafunzi na baina ya wanafunzi ili wanafunzi waweze kuzingatia masomo yao na kufaulu mitihani yao.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Sehemu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Bwana Makwasa Bulenga amemshukuru Katibu Tawala wa Mkoa kwa kutenga muda na kuzungumza na Wakuu wa Shule ambao ni wadau muhimu katika usimamizi wa Elimu ya Sekondari.
Bwana Makwasa ameeleza kuwa anategemea mabadiliko makubwa baada ya kikao hicho katika usimamizi na uendeshaji wa shule za Sekondari katika Mkoa wa Mara.
Bwana Makwasa amewashukuru walimu pamoja na changamoto zilizopo katika shule zao wamekuwa wakitafuta ufumbuzi hususan katika kupata walimu wa kujitolea na kutoa taarifa ya upungufu au uchakavu wa miundombinu katika Halmashauri zao.
Kikao hicho kilihudhuliwa pia na Katibu Tawala Wilaya ya Musoma, baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Maafisa Elimu wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa