Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu leo amezindua kituo cha kuratibu usafiri wa dharura kwa wajawazito, wazazi na watoto wachanga (M-MAMA) kwa Mkoa wa Mara katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la Kwangwa, Manispaa ya Musoma.
Akizungumza baada ya kuzindua kituo hicho, Bwana Msalika Makungu amewataka watumishi wa sekta ya afya watakaoratibu mfumo huo kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa uadilifu ili kupunguza na hatimaye kutokomeza kabisa vifo vya Mama na Matoto vinavyotokana na kucheleweshwa kupata huduma za matibabu.
“Pamoja na uwekezaji mkubwa ambao serikali imefanya katika kujenga miundombinu, kununua dawa na vifaa tiba, kuajiri na kuwamotisha watumishi katika sekta ya afya, kama hatutafanya kazi kwa kuzingatia maadili, uadilifu na kuthamini uhai wa watu, vifo vitaendelea kuwepo” alisema Bwana Makungu.
Aidha, Bwana Msalika amezitaka Kamati za Usimamizi wa Afya katika ngazi za Mkoa na Halmashauri kuhakikisha mfumo huo unasimamiwa vizuri na unaleta matokeo chanya katika maisha ya wananchi wa Mkoa wa Mara.
Bwana Makungu amewataka wananchi kuitumia namba 115 ya kuomba usafiri kwa kuzingatia madhumuni ya namba hiyo na hitaji la msingi la kuwasaidia wagonjwa wenye uhitaji wa dharura ili kuweza kuokoa maisha ya Mama na Mtoto.
Akizungumza katika tukio hilo, Muuguzi Mkuu na Mratibu wa M-MAMA Mkoa wa Mara Bwana Stanley Kajuna ameeleza kuwa mpango wa M-Mama katika Mkoa wa Mara umezinduliwa rasmi tarehe 13 Februari, 2023 na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee.
Bwana Kajuna ameeleza kuwa baada ya uzinduzi shughuli mbalimbali zimefanyika kuruhusu maandalizi ya kuanza kutumika kwa mfumo huo ikiwa ni pamoja na kutambua magari na madereva wa jamii watakaotoa huduma, kuwafanyia mafunzo madereva na kuingia nao makubaliano rasmi.
Aidha, shughuli nyingine ilikuwa kuwatambua na kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa mfumo, kuandaa chumba maalum kitakachotumika kuratibu usafiri wa dharura na kuweka nyenzo muhimu katika uratibu wa mfumo huo.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na wawakilishi wa Vodacome Tanzania Foundation, Pathfinder International, Touch Foundation, wawakilishi wa Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na baadhi ya wasimamizi wa mfumo huo kutoka Mkoa wa Mara.
M-MAMA ni mfumo wa Serikali ulioandaliwa kusaidia upatikanaji wa usafiri wa haraka wakati wa dharura wa kusafirisha wajawazito, wazazi na watoto wachanga wenye changamoto kutoka kituo kimoja kwenda kingine ili kupata matibabu zaidi ambayo hayawezi kupatikana katika kituo cha awali.
Mkoa wa Mara unakuwa Mkoa wa 17 kuanza kutumia mfumo huu tangu mfumo huu ulipozinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 6 Aprili, 2023 Mkoani Dodoma na kuagiza mfumo huu kutumika nchi nzima.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa