Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu leo amefungua rasmi mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu Wakuu wa Shule za Msingi kutoka Halmashauri tano za Mkoa wa Mara yanayofanyika katika Chuo cha Ualimu Bunda na kuwataka Walimu Wakuu kusaidia kuboresha elimu ya msingi hapa nchini.
Bwana Makungu amewataka Walimu Wakuu kutumia mafunzo haya waliyopewa na Mradi wa BOOST kuboresha utendaji, uongozi na usimamizi wao katika miradi ya elimu na kuacha kufanyakazi kwa mazoea.
“Uongozi sio kazi rahisi sana, ukiiona rahisi basi wewe utakuwa hufanyi kinachotakiwa kufanyika, uongozi ni dhamana na mafunzo haya yawasaidie katika kuboresha utendaji, usimamizi na uongozi wenu katika shule zenu, tuone mabadiliko” amesema Bwana Makungu.
Bwana Makungu ameeleza kuwa kama Walimu Wakuu wakitimiza wajibu wao vizuri, maboresho katika elimu yataonekana kwa wazi na watu watajua kuwa shule zinazongozwa na viongozi walioiva vizuri na kusimamia ufundishaji, watumishi, rasilimali na miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Bwana Makungu, Serikali imeboresha miundombinu, idadi ya walimu na watumishi, mishahara na madai mbalimbali yamelipwa vizuri kinachohitajika kikubwa ni Walimu Wakuu wenye kujituma na kuonyesha mfano katika kusimamia ili kama Taifa tuweze kunufaika na uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu.
Aidha, amewataka Walimu Wakuu kuwashirikisha kuhusu miradi, mipango na bajeti watumishi wote walio chini yao ili kupata uungwaji mkono katika utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyopo katika Shule za Msingi na kuacha kuwa na makundi ya watumishi katika shule hizo.
Bwana Makungu amewataka Walimu Wakuu kutoa taarifa kwa viongozi wa Halmashauri na Mkoa wanapoona wanaingiliwa katika manunuzi ya vifaa na utendaji wao wa kila siku na viongozi au watu wengine nje ya mfumo wa elimu.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bibi Judith Mrimi amesema amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa afua namba nne ya mradi wa BOOST ambayo inalenga kuboresha uongozi na usimamizi katika elimu.
Bibi Mrimi amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuboresha uongozi, usimamizi na uendeshaji wa Shule za Msingi katika Mkoa wa Mara na kuwaomba walimu kujifunza na baadaye kuyafanyia kazi mafunzo waliyopewa.
Mafunzo hayo kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi yametolewa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa BOOST na kutolewa na wakufunzi kutoka Chuo cha Uongozi wa Elimu, Bagamoyo (ADEM) na Maafisa Elimu Taaluma wa Halmashauri zilizohusika.
Mafunzo hayo ya siku tatu kwa awamu ya kwanza yamewahusisha Walimu Wakuu 415 kutoka Shule za Msingi kutoka Halmashauri za Mji wa Bunda, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na Manispaa ya Musoma.
Kwa awamu ya pili mafunzo kama hayo yatafanyika katika Mji wa Tarime na kuwahusisha walimu Wakuu kutoka Shule za Msingi za Halmashauri za Tarime Mji, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Ufunguzi wa mafunzo hayo umehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda Bwana Salum Mtelela, Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Mara Bwana Adam Janga, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Bunda, wakufunzi kutoka ADEM na Maafisa Elimu Taaluma wa Halmashauri zilizohusika.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa