Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu amewataka viongozi wa Mkoa wa Mara kushiriki kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi na wadau wengine kushiriki kutoa maoni katika uandaaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025/2050.
Akizungumza katika ufunguzi wa warsha ya kuhamasisha ushiriki wa wadau katika maandalizi ya Dira hiyo, Bwana Makungu ameeleza kuwa warsha hiyo imelenga kutoa elimu kwa viongozi na wawakilishi wa makundi ya wadau kuhusu dira hiyo na utekelezaji wake pamoja na mchakato wa maandalizi ya Dira ya 2050.
“Mnapaswa kushiriki kikamilifu katika warsha hii kwa lengo la kuwa na uelewa wa pamoja na kuelewa majukumu yenu ya msingi ili kufanikisha shughuli hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu” amesema Bwana Makungu.
Bwana Makungu amesema kuwa wajumbe wa timu ya uandishi watasambaza nakala za vitabu vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, vipeperushi, mabango kuhusu maandalizi ya Dira 2050 na kutembelea vyombo vya habari vilivyopo katika Mkoa wetu nah ii itasaidia kuongeza wigo wa watu watakaofikiwa pamoja na kuacha nyenzo zitakazosaidia kuendelea na uelimishaji wa umma.
Kwa upande wake, Bwana Servus Sagday, Kiongozi wa Timu ya Uandishi wa Dira 2050 kwa Kanda ya Ziwa amewataka viongozi kuelewa maana na umuhimu wa Dira na kusaidia katika utoaji wa elimu kwa wananchi wanaowaongoza katika maeneo yao.
“Ili kupata ushiriki wa wananchi wengi katika maandalizi ya Dira 2050 ni muhimu kwa viongozi kuwapa elimu kuhusu Dira 2050 na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa wananchi kushiriki ili kupata Dira itakayogusa maisha ya Watanzania wote” amesema Bwana Sagday.
Kwa upande wake Bwana Peter Soke, mjumbe wa timu ya Uandishi wa Dira 2050 ameesa kuwa katika kupata maoni ya wadau njia mbalimbali zitatumika ikiwa ni pamoja na madodoso, mahojiano ya vikundi, vikao vya majadiliano na mahojiano maalum na baadhi ya watu.
“Ili kupata maoni ya wadau wengi zaidi tutatumia pia mitandao ya simu na online portal ili kuwawezesha wananchi wengi kutoka maeneo mbalimbali kushiriki na kutoa maoni kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050” amesema Bwana Soke.
Bwana Soke ameeleza kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa inayotumika sasa ilianza mwaka 2000 hadi 2025 ikiwa na lengo kubwa la kuiwezesha Tanzania kuingia Uchumi wa Kati na Maisha bora kwa Kila Mtanzania na kuongeza kuwa kwa kiasi kikubwa Dira hii ilifanikiwa.
Ameeleza kuwa lengo la kuandaa Dira mpya ni kuendeleza malengo ya awali, kupata mwelekeo na mpango wa Taifa na ili kuendana na mabadiliko mbalimbali yaliyopo na yanayotarajiwa katika jamii kwa kipindi hicho.
Bwana Soke amewataka viongozi walioshiriki katika mkutano huo kushiriki katika kutoa elimu kwa wananchi na zoezi la ukusanyaji wa maoni ya wananchi katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Mara Bwana Iddi Hamisi Mtani ameeleza kuwa ili kupata maoni ya watu wenye ulemavu, mbinu mbalimbali zinatakiwa kutumika ili kuwawezesha watu wenye ulemavu kuweza kutoa maoni.
Bwana Mtani amesema watahitajika wakalimani kuwasaidia watu wenye ulemavu wa kusikia, maandishi ya nukta nundu na maandishi manene kwa walemavu wenye matatizo ya kuona, kuangalia mazingira rafiki ya kuhojiwa kwa walemavu wa viungo na ngozi.
“Inafaa kuangalia mahitaji halisi ya watu wenye ulemavu na kuyajumuisha katika mipango ya jumla ya maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Taifa 2050 kutokana na changamoto mbalimbali za watu wenye za walemavu” amesema Bwana Mtani.
Warsha ya kutoa elimu kwa viongozi ilihudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Sehemu na Vitengo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na baadhi ya wakuu wa idara za Halmashauri.
Wengine waliohudhuria warsha hiyo ni viongozi wa dini, vyama vya siasa, viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu na mashirika yasiyo ya kiserikali na waandishi wa habari.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa