Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu leo amefanya kikao na wasimamizi wa afya katika Halmashauri na Wakuu wa Vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara na kuwataka kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya afya.
Akizungumza katika kikao hicho Bwana Makungu ameeleza matamanio yake kuwa Mkoa wa Mara uwe Mkoa wa mfano katika utoaji wa huduma bora za afya na mikoa mingine waje kuiga Mara.
“Sisi tuwe Mkoa ambao unatoa huduma bora za afya, huduma nzuri na kwa wakati, lugha nzuri kwa wagonjwa, tufanye kazi kama timu moja ili kuondoa changamoto mbalimbali zinazotukabili na kujenga uhusiano mzuri katika maeneo yetu ya kazi, tutafanikiwa” amesema Bwana Makungu.
Bwana Makungu amewataka wasimamizi na wakuu wa vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara kutimiza wajibu wao ili kuwa wa mfano kwa watumishi waliochini yao na kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya havigeuki kuwa vituo vya malalamiko ya wananchi.
Aidha, Bwana Makungu amewahimiza watumishi woe wa sekta ya afya kuisaidia Serikali katika kutekeleza sheria ya mtoto ambayo inapiga marufuku vitendo vya ukeketaji katika jamii ili kuwanusuru watoto wakike kutokana na ukeketaji.
Bwana Makungu amewahimiza watumishi kuzijua sheria za utumishi wa umma ili kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.
Katibu Tawala amewahimiza wasimamizi wa sekta ya afya na wakuu wa vituo vya kutolea huduma za afya kutoa elimu kwa wananchi wote kuhusiana na umuhimu wa Bima ya Afya ili wananchi waweze kujiunga na kupata huduma za afya kwa urahisi zaidi.
Wakati huo huo, Bwana Makungu amewataka wasimamizi wa sekta ya afya kuhakikisha mifumo ya kukusanya mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya inafungwa sehemu zote muhimu na inafanyakazi ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Zabron Masatu amemshukuru Katibu Tawala kwa kutenga muda wake kuzungumza na wasimamizi wa sekta ya afya na kuahidi kuyafuatilia mambo yote yaliyozungumzwa katika kikao hicho.
Akizungumza kuhusiana na rasimu ya Mfuko ya Bima ya Afya kwa wote, Dkt. Masatu amesema mfuko huu utakuwa ni mkombozi wa watanzania walio wengi katika kupata huduma za afya za uhakika wakati wote wanapohitaji.
Dkt. Masatu amewataka wasimamizi wa afya katika Halmashauri kutoa elimu kuhusu mpango wa serikali kwa wananchi ili waweze kuelewa na kuchukua hatua za kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha huduma za afya.
Katika kikao hicho pia watumishi walipata nafasi ya kusikilisha wasilisho la Shiria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma na rushwa katika mazingira ya kazi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa