Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu leo tarehe 5 Agosti, 2022 amewasili na kukabidhiwa ofisi na baadaye kuzungumza na Wakuu wa Vitengo na Idara pamoja na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara katika Ukumbi wa Uwekezaji.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na Wakuu wa Vitengo na Idara na wafanyakazi wakati wa makabidhiano hayo, Bwana Msalika amewahimiza wafanyakazi kutoa ushirikiano baina yao na kati yao na viongozi katika utekelezaji wa majukumu.
“Ninaomba tuendelee na ushirikiano uliopo na ili tutekeleze majukumu yaliyo mbele yetu kwa ufanisi katika kuzisimamia Halmashauri za Mkoa wa Mara” alisema Bwana Msalika.
Bwana Msalika ameeleza kuwa kwa sasa kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kuongeza makusanyo ya ndani ya Halmashauri na kuwataka wafanyakazi kusimamia kwa weledi makusanyo ya Halmashauri.
Aidha, Bwana Msalika amewataka wafanyakazi kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Kwa upande wake, aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela amewashukuru wafanyakazi wa Mkoa wa Mara kwa ushirikiano wao katika kutekeleza majukumu.
“Ninawashukuru sana kwa ushirikiano mlionionyesha wakati wote nilipokuwa hapa, ninawaomba muendelee na ushirikiano huo kwa Katibu Tawala mpya ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa urahisi zaidi” alisema Bwana Msovela
Katika tukio hilo, Bwana Msovela alimkabidhi ofisi Bwana Msalika tukio ambalo lilitanguliwa na kikao cha Katibu Tawala na Wakuu wa Idara na Vitengo na baadaye kikao na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Aidha, katika tukio hilo wafanyakazi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa ametoa zawadi kwa Bwana Msovela na wamemkaribisha Bwana Msalika ambaye amewasili leo.
Bwana Msalika aliteuliwa na Rais tarehe 28 Julai, 2022 kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara ambaye anachukua nafasi ya Bwana Albert Gabriel Msovela ambaye amehamishiwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa