Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu leo amegawa magari matatu kwa Hospitali ya Rufaa Kubukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kwangwa) na Chuo cha Maafisa Tabibu Musoma yaliyotolewa na serikali yenye lengo la kuboresha usimamizi wa Sekta ya Afya.
Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo, Bwana Makungu amewataka wahusika kutumia magari hayo kwa mujibu wa maelekezo ya matumizi yake yaliyokusudiwa na Serikali.
“Ni mategemeo ya Serikali kuwa magari haya yatatumika kama ilivyokusudiwa na yataimarisha utoaji wa huduma katika Sekta ya Afya” amesema Bwana Makungu.
Bwana Makungu amesema gari moja la kisasa la kubebea wagonjwa na gari moja la usimamizi yametolewa kwa ajili ya Hospitali ya Kwangwa wakati gari moja ya usimamizi imetolewa kwa ajili ya Chuo cha Maafisa Tabibu Musoma.
Bwana Makungu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Afya na Serikali kwa ujumla kwa kuuwezesha Mkoa wa Mara kwa vitendea kazi .
Aidha, Bwana Makungu ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya tayari imeshanunua magari mengine mawili kwa ajili ya Hospitali ya Kwangwa ambayo yatafika muda wowote kuanzia sasa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Maafisa Tabibu Musoma Dkt. Agustine Johnson ameishukuru Serikali kwa kukipatika Chuo hicho gari jipya ambalo amesema litaongeza nguvu katika ufundishaji wa mafunzo kwa vitendo.
“Kwa sasa Chuo kina gari moja tu na tuna wanachuo 400 ambao mara kwa mara wanahitaji kufanya mafunzo kwa vitendo katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya pamoja na kufuatilia mitihani ya wanachuo gari hili lilikuwa halitoshi” amesema Dkt. Johnson.
Dkt. Johnson ameiomba Serikali kukinunulia Chuo hiki basi dogo ili kurahisisha ufanyaji wa mafunzo kwa vitendo kwa wanachuo.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere amesema kuwa hospitali ilikuwa inachangamoto ya gari la kubebea wagonjwa lenye uwezo wa kwenda umbali mrefu kama vile Dodoma au Dar es Salaam na sasa gari hii wanategemea kuitumia kwa ajili hiyo.
Aidha, amesema gari hiyo ya wagonjwa ni ya kisasa na imewekewa vifaa tiba, mifumo ya gesi na inauwezo wa kufanya upasuaji mdogo kwa mgonjwa gari ikiwa njiani na hivyo kuokoa maisha ya wagonjwa wakiwa wanasafirishwa kwenda kwenye matibabu ya rufaa.
Aidha, amesema gari ya usimamizi itatumika kutembelea vituo vya kutolea huduma vilivyopo ili kutoa utaalamu na ushauri kwa watoa huduma waweze kuboresha utoaji wa huduma za afya.
Magari yaliyotolewa ni sehemu ya magari 31 ambayo Mkuu wa Mkoa wa Mara aliyatolea taarifa tarehe 23 Novemba, 2023 kuhusiana na mgao wa magari na vifaa tiba na baadhi ya magari hayo bado hayajapokelewa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa