Makabidhiano ya mali za uliokuwa ushirika wa Mara Cooperative Union 1994 Ltd kwa vyama vya ushirika vya mazao ya pamba na kahawa yamefanyika leo katika Kiwanda cha Kuchambua Pamba na Mafuta ya Pamba cha Mgango katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mufilisi wa Ushirika huo Bwana Juma Shaaban Mrisho ameeleza kuwa mali zinazokabidhiwa ni pamoja na viwanda vinne vya mazao vyenye thamani ya shilingi bilioni 5.2 na madeni ya zaidi ya shilingi bilioni 10.5.
“Madeni haya yanajumuisha madeni ya chama cha Ushirika cha Mara Cooperative Unioni 1994 Ltd ikiwemo mkopo kutoka Benki ya Biashara (NBC), madai ya watumishi na madeni kwa taasisi mbalimbali na madeni yaliyotokana na shughuli za ufilisi.
Bwana Mrisho ameeleza kuwa mali nyingine za ushirika huo ni Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe iliyopo katika Manispaa ya Musoma yenye thamani ya shilingi milioni 550 ambayo Serikali iliichukua na kuanzisha Shule ya Sekondari ya Wasichana.
Aidha, Bwana Mrisho ameeleza kuwa katika kipindi chote walichofanya kazi ya ufilisi wa ushirika huo tangu mwaka 1996 walifanikiwa kukusanya shilingi bilioni 1.9 ambazo zilitumika katika shughuli za ufilisi wa ushirika huo kuanzia wakati huo hadi tarehe 12 Desemba, 2022.
“Kutokana na kuchelewa zoezi la makabidhiano, zoezi la ufilisi lilikuwa likizalisha madeni kila mwaka, viwanda kuchakaa na kupungua thamani na wananchi kuvamia maeneo ya viwanda vinavyomilikiwa na ushirika huo ndio baadhi ya changamoto tulizokabiliana nazo” alisema Bwana Mrisho.
Kwa upande wake, Mrajisi wa Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege ameeleza kuwa mgawanyo wa mali na madeni kwa vyama hivyo umetegemea zaidi mazao wanayoshughulika nayo.
Ameeleza kuwa katika mgawanyo huo, WAMACU wanapata Kiwanda cha Kawaha cha Tarime, ardhi ya kiwanda hicho na asilimia 20 ya deni lote lililobakia wakati PMCU inapata viwanda vya pamba vya Mugango (Musoma), Kibara na Rushashi (Bunda) pamoja na ardhi ya viwanda hivyo na mali zilizomo na madeni asilimia 80.
Aidha, Bwana Ndiege ameeleza kuwa madeni hayo bado yanaendelea kuhakikiwa uhalali wake na Ofisi ya Mrajisi utasimamia kuhakikisha madeni yote yanalipwa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gambaless Timotheo ameeleza kuwa urejeshaji wa mali hizo za ushirika utasaidia kuchochea ukuaji wa kilimo cha mazao ya pamba na kahawa katika Mkoa wa Mara.
“Ni matumaini yangu mtakuja na mkakati madhubuti wa kuendeleza viwanda hivi na kuzitunza mali za ushirika mlizokabidhiwa leo kwa manufaa ya wanaushirika wote wa Mkoa wa Mara” alisema Bwana Timotheo.
Bwana Timotheo ameipongeza Ofisi ya Mrajisi na Mufilisi kwa kusimamia zoezi hilo vizuri na kuhakikisha vyama hivyo vinapata mali zao zikiwa salama na makabidhiano yanafanyika kwa amani.
Wakati huo huo, Bwana Timotheo amevipongeza WAMACU na PMCU kwa kuonyesha tija katika kipindi kifupi na kuwezesha kuaminiwa na Serikali na kuvitaka vyama hivyo kuvirejesha viwanda vyote katika uzalishaji ili wananchi wapate soko la kuuzia mazao yao kwa urahisi.
Bwana Timotheo ameeleza kuwa Mkoa wa Mara katika msimu huu wa kilimo umepanga kupata tani 25,000 za kahawa na tani 80,000 za pamba lakini anatarajia baada ya makabidhiano hayo na viwanda kuanza kufanyakazi kutakuwa na mapinduzi ya kilimo cha mazao hayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Kahawa Mkoa wa Mara (WAMACU LTD) Bwana David Mwita Hechei ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kuzitoa mali za ----kwa ushirika wao na kuahidi kuzitumia mali hizo kama mtaji wa kuendeleza shughuli za ushirika.
Bwana Heichei ameiomba Serikali katika ngazi zote kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyama hivi vya ushirika vilivyokabidhiwa mali na madeni kuhakikisha vinaendelea kufanya shughuli zake kwa maendeleo ya wanaushirika.
Aidha, ameiomba serikali kurejesha mali za vyama vya msingi vya ushirika zilizokabidhiwa kwa Serikali za Vijiji ili vyama vya ushirika vya msingi viweze kupata mali hizo ili kuviendeleza.
Bwana Heichei ameiomba Serikali kuendelea na uhakiki wa madeni waliyokabidhiwa ili vyama hivyo vilipe madeni yake halali tu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Pamba Mara Cooperative Union (PMCU) Bwana Daudi Kisingi Iramba ameeleza kuwa leo ni siku ya furaha sana kwa kuwa baada ya miaka 26 mali za wanaushirika zimerudi kwa wanaushirika wa Mkoa wa Mara.
Bwana Iramba ameahidi kuandaa mpangokazi wa vyama vyao vya ushirika na kuukamilisha kabla ya tarehe 1 Januari, 2023 kama walivyoelekezwa na kuuwasilisha Ofisi ya Mrajisi kwa hatua zaidi.
Aidha, Bwana Iramba ameahidi kuwa viwanda walivyokabidhiwa vitaanza kufanyakazi mara moja kwa maendeleo ya wanaushirika na wananchi wote wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa