Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa leo ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama iliyopo katika Kijiji cha Butiama kwenye eneo lenye ofisi za Serikali.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi, Mhe. Majaliwa amepongeza mradi huo na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuleta fedha katika Wilaya ya Butiama kwa sababu ni wilaya mpya na nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mhe. Majaliwa ameitaka TBA kukamilisha mradi huo kwa haraka ili kuboresha mazingira ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama na pia aweze kuhamia katika eneo hilo lenye ofisi nyingine zote za Serikali.
Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mkuu amempongeza Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Jumanne Sagini kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika jimbo hilo.
Akizungumza wakati wa kuwasalimia wananchi wa Wilaya ya Butiama Mhe. Waziri Mkuu amewashukuru wananchi na viongozi wa Wilaya ya Butiama kwa mapokezi mazuri.
Akitoa taarifa za mradi huo, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhandisi Richard Moshi ameelza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ilitenga fedha kwa ajili ya mradi huo kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 na huendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya ujenzi huo.
Eng. Moshi ameeleza kuwa mradi huo umeanza kutekelezwa tarehe 5 Agosti, 2022 na Mkandarasi wa mradi huo ni Wakala ya Majengo (TBA) kwa gharama ya shilingi 2,041,935,338.32 na muda wa mradi ulikuwa ni miezi 12 hata hivyo muda wa utekelezaji wa mradi huo uliongezwa.
Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 60 na mpaka wakati huu mkandarasi ameshalipwa shilingi 843,394,728.35 ikiwa ni malipo ya awali na hati za malipo ya pili na ya tatu huku hati ya nne ikiwa imetumwa Hazina kwa ajili ya malipo.
Mhandisi Moshi ameeleza kuwa mradi huo una changamoto ya kasi ndogo ya mkandarasi katika utekelezaji wa mradi inayosababishwa na uwezo mdogo wa kifedha wa mkandarasi hivyo kushindwa kufuata mpangokazi uliowekwa.
Kwa upande wake, Mhe. Sagini amesema yapo mambo mengi yamefanyika katika Wilaya ya Butiama katika miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, Chuo Kikuu cha Butiama na Chuo cha VETA kilichojengwa katika jimbo la Butiama.
Mhe. Sagini amesema ukarabati wa majengo ya awali ya Chuo kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere Butiama ukarabati umekamilika, wanafunzi wameanza masomo kwa mwaka huu wa masomo na serikali kupitia mradi wa maendeleo ya Vyuo Vikuu unaofadhiliwa na benki ya Dunia imetoa zaidi ya bilioni 100 na kwa sasa ujenzi umeanza.
Akiwa Butiama, Mhe. Majaliwa pia amefanya kikao na watumishi na madiwani, ametembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kupokelewa na wanafamilia, amewasalimia wananchi na kuendelea na ziara yake Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa