Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) leo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara ACP Salum Morcase kuwakamata Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Mfanyabiashara wa Serengeti aliyeshiriki katika wizi wa fedha za Serikali zaidi ya shilingi milioni 213.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Majaliwa amewataja waliohusika na wizi wa fedha hizo kuwa ni pamoja na Bwana Saad Katunzi Shabailu Mwekahazina wa Halmashauri ya Serengeti na mfanyabiashara wa Mji wa Mugumu Bwana Daudi Matinde ambao baada ya kuhojiwa na timu kutoka ofisi ya Waziri Mkuu walikili kuhusika katika tukio hilo.
“Katika wizi huo, Mkurugenzi wa Halmashauri, Baraza la Madiwani, viongozi wa TAMISEMI hawakuwa na taarifa za wizi huo kwa sababu umefanywa katika mtandao unaowahusisha watumishi wa tatu wa TAMISEMI kutoka Kitengo cha Treasury Single Account (TSA)” amesema Mhe. Majaliwa.
Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa tarehe 10 Juni, 2023 walitumia mwanya wa kuiombea kibali fedha ya bakaa kwa barua iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwenda hazina, na ilipofika tarehe 30 Juni,2023 walikuwa wameshamaliza matumizi ya fedha iliyoombewa kibali.
Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa baada ya kufanikiwa kutoa fedha hizo Bwana Ishabailu alipanda basi hadi kituo cha mabasi cha Nyegezi Jijini Mwanza na kukabidhi shilingi milioni 150 kwa Bwana Zabron Mponzi ambaye alisema fedha hizo zilikuwa zinahitajika haraka kwa wakubwa Dodoma nay eye akapewa shilingi milioni 39.
Mhe. Majaliwa amelitaka Baraza la Madiwani kuwa makini katika matumizi ya fedha za Serikali na kuwasimamia watumishi wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limemkamata Bwana Shabailu wakati kikao cha Waziri Mkuu na watumishi pamoja na viongozi wa Wilaya ya Serengeti kikiwa kinaendelea kwa ajili ya kwenda kumfungulia mashtaka.
Akiwa Serengeti, Mhe. Majaliwa amefanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Sokoine mjini Mugumu na kuelekea Wilaya ya Tarime ambapo amezungumza na wananchi wa Nyamwaga katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Baada ya Hapo Mhe. Waziri Mkuu kesho atafanya ziara katika Wilaya ya Rorya na kuhitimisha katika Wilaya ya Tarime ambapo atafanya mikutano katika eneo la Sirari na katika uwanja wa Serengeti Tarime Mjini.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa