Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli ameidhinisha shilingi bilioni 33.9 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wakazi 1,639 wa vijiji viwili vinavyouzunguka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara katika Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara.
Malipo ya fidia hizo yameanza kulipwa leo tarehe 20 Mei 2020 kama ilivyoahidiwa awali na Mkuu wa Mkoa wa Mara na kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Madini Mheshimiwa Dotto Biteko.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa malipo ya fidia kwa wananchi hao, Mheshimiwa Biteko ameeleza kuwa tarehe 7 Septemba 2018 Rais alipotembelea Nyamongo aliagiza serikali kutatua kero mbili za wananchi wa Nyamongo ambazo ni malipo ya fidia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika eneo hilo.
“Leo nimekuja hapa kuwaeleza kuwa kero hizi zote mbili serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Magufuli imezitatua” alisema Mheshimiwa Bitteko.
Aidha ameeleza kuwa kwa sasa serikali imekuwa ikifaidika sana na mauzo ya madini kupitia masoko ya madini yaliyopo hapa nchini. Akitolea mfano wa eneo la Nyamongo Mheshimiwa Biteko ameeleza kuwa awali kabla ya kufungua soko la madini serikali ilikuwa inapata fedha kidogo sana lakini kwa sasa mapato yameongezeka maradufu.
Akizungumza wakati akiwakaribisha waheshimiwa mawaziri kuzungumza na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameeleza kuwa malipo haya ni utatuzi wa kero ya muda mrefu sana ya wananchi wa Nyamongo.
“Suala la kulipa fidia kwa wananchi hawa ni katika matatizo sugu na lilikuwepo kwa zaidi ya miaka 11 mpaka sasa” alisema Malima.
Mheshimiwa Malima alisema anashukuru ushirikiano ulioonyeshwa na Wizara ya Madini pamoja na Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Mgodi wa Barrick North Mara katika kutatua kero hiyo ya muda mrefu.
Kwa upande wake Diwani wa Nyamongo Mheshimiwa Rashid Bongomba ameeleza kuwa awali wananchi walikuwa na matatizo mengi na mgodi hapo lakini sana mengi yametatuliwa ilibakia hili la fidia tu kwa wananchi.
“Kwa fidia hii, serikali imesaidia wananchi kurudisha imani yao kwa Chama cha Mapinduzi, na ninawahakikishia kuwa matokeo yake tutayaona” alisema Mheshimiwa Bongomba.
Aidha aliomba viongozi wa serikali kuangalia uwezekano wa kuleta barabara ya lami Nyamongo ili kutatua kero ya usafiri ya muda mrefu kwa wananchi wa eneo hilo.
Uzinduzi wa kulipa fidia kwa wananchi ulihudhuriwa pia na Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu; Naibu Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Serikali Mheshimiwa Angelina Mabula na viongozi wengine wa chama na serikali.
Wananchi 1639 wa vijiji vya Nyabichune na Matongo katika eneo la Nyamongo wamelipwa fidia zao kupitia katika akaunti zao za benki.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa