Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee ameeleza kuwa maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 katika Mkoa wa Mara yamekamilika.
Akizungumza katika matangazo ya moja kwa moja yaliyorushwa kupitia Kituo cha Redio cha Bunda FM leo, Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa tayari Makarani wa Sensa wapo katika maeneo yao ya kazi na wanaendelea na maandalizi ya kuanza zoezi saa sita usiku wa kuamkia kesho tarehe 23 Agosti, 2022.
“Maandalizi yote muhimu ya Sensa kwa Mkoa wa Mara yamekamilika, na tayari makarani wapo katika vituo na Wasimamizi wa Sensa wanaendelea kupokea changamoto na kuzitatua kwa kadiri zinavyoendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu sura ya 351, taarifa zote zitakazotolewa na wananchi kwa karani wa Sensa zitakuwa ni siri na zitatumika kwa madhumuni ya Sensa na makarani wote wamesaini kiapo cha kutunza siri za taarifa zote atakazozikusanya katika zoezi la Sensa.
“Karani yeyote akithibitika kwenda kinyume na kiapo cha kutunza siri, atashtakiwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria hii, hivyo ninaomba kuwahakikisha wananchi kuwa taarifa watakazozitoa kwa karani wa Sensa zipo salama na hivyo niwaombe watoe taarifa sahihi ili Serikali ipate takwimu sahihi” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee ambaye aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu, ameeleza kuwa makarani wa sensa wakienda kuhesabu watu wataambatana na viongozi wa serikali ya mtaa au vitongoji wa eneo husika.
Mheshimiwa Mzee amewaomba wananchi wote wa Mkoa wa Mara kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi la mwaka 2022, kutoa taarifa sahihi kwa makarani wa Sensa na wazazi/walezi wa Watoto/watu wenye ulemavu kuhakikisha watu wote wenye ulemavu wanahesabiwa.
“Hii itaiwezesha Serikali kutambua idadi ya watu wenye ulemavu katika kila eneo, aina ya ulemavu, msaada unaohitajika na namna bora ya kuweza kuwasaidia mmoja mmoja au kama kundi la watu wenye ulemavu” alisema Mheshimiwa Mzee.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa