Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameeleza kuwa maandalizi ya maonyesho ya kilimo ya NANENANE kwa mwaka 2020 yatakayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyakibindi katika Mkoa wa Simuyu yamekamilika.
Mheshimiwa Malima ameeleza hayo leo tarehe 25 Julai 2020 katika kikao cha pamoja kati ya maafisa wa serikali wa mikoa ya Kanda ya Ziwa Mashariki na wadau wa maonyesho hayo kilichofanyika katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.
“Mpaka sasa sehemu kubwa ya maandalizi haya yapo vizuri na tunaendelea kukamilisha shughuli ndogondogo zilizobakia na tunatarajia tarehe 30 Julai 2020 maonyesho haya yataanza hapa Nyakabindi” alisema Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima ambaye kwenye kikao hicho alikuwa Kaimu Mwenyekiti amemtaka Katibu Tawala Msaidizi, Miundombinu wa Mkoa wa Simiyu kuhakikisha anakamilisha shughuli za kuleta huduma za maji, umeme na barabara kabla ya tarehe 29 Julai 2020.
Aidha ameelezea matarajio yake kuwa Waziri wa Kilimo ataongeza mwaka mmoja zaidi kwa Kanda ya Ziwa kuendelea kuandaa maonyesho haya katika uwanja huu wa Nyakabindi.
Aidha amewakaribisha wadau wote wa maonyesho kuja kuanzia tarehe 30 Julai 2020 ili kujionea na kujifunza shughuli mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Zainab R. Telak ameeleza kuwa kazi ya maandalizi ya nanenane iliyofanyika mpaka sasa ni nzuri sana.
“Kutokana na janga la Corona tulikuwa na wasiwasi lakini kila kitu kimeenda sawa na wadau wengi sana wanashiriki mwaka huu” alisema Mheshimiwa Telak.
Ameeleza kuwa tayari vipando vipo katika hali nzuri na mabanda yanaendelea kujengwa na michango ya wadau inaendelea kupokelewa hivyo bado tu kuyafungua rasmi ili wananchi waweze kupata huduma uwanjani hapo.
Maonyesho ya Nanenane kwa mwaka 2020 yanafanyika katika uwanja wa Nyakabindi Mkoani Simiyu na yanatarajiwa kuanza tarehe 30 Julai 2020 lakini ufunguzi rasmi utafanywa tarehe 1 Agosti 2020.
Waandaaji wakuu wa maonyesho haya ni mikoa inayounda Kanda ya Ziwa, Mashariki ambayo ni Simiyu, Mara na Shinyanga.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa