Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu leo ametoa taarifa ya maandalizi ya mapokezi na mbio za Mwenge wa Uhuru katika kikao cha maandalizi ya Mwenge wa Uhuru Mkoa wa Mara na kuwahakikishia wajumbe kuwa maandalizi yamekamilika.
Bwana Makungu ameeleza kuwa ukiwa katika Mkoa wa Mara Mwenge wa Uhuru utakagua, kuzindua na kutembelea miradi ya maendeleo 63 yenye thamani ya shilingi 17,258,727,862.80
“Miradi hii 63 iko katika halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara na kugharimiwa na michango ya wananchi, Halmashauri, Serikali Kuu na wahisani wa maendeleo” amesema Bwana Makungu.
Bwana Makungu ameeleza kuwa miradi ya maendeleo itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru itatoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti (7), Halmashauri ya Wilaya ya Butiama (6), Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (7), Halmashauri ya Mji wa Tarime (6) Halmashauri ya Wilaya ya Rorya (8) na Manispaa ya Musoma (7).
Kwa mujibu wa Bwana Makungu miradi mingine inatoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (7), Halmashauri ya Mji wa Bunda (8) na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda (7).
Kwa upande wake Mratibu wa Mbio za Mwenge, Mkoa wa Mara Bwana Fidel Baragaye imeeleza kuwa Mwenge wa Uhuru utapokelewa katika viwanja vya Shule ya Msingi Robanda, katika Kijiji cha Robanda, Kata ya Ikoma katika Hifadhi ya Jamii ya Ikona (Ikona WMA) iliyopo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti tarehe 4 Julai, 2023.
Bwana Baragaye ameeleza kuwa katika Mkoa wa Mara Mwenge wa Uhuru utakagua,kuzindua, kutembelea na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya afya, elimu, maji, barabara, madaraja, vikundi vya uzalishaji mali vya vijana na kufanya mikutano ya kuwaelimisha wananchi.
“Miradi itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru imegharimiwa na michango ya wananchi 2,212,111,700/=, fedha za Halmashauri 1,351, 300,345/=, fedha kutoka Serikali Kuu 9,747,566,042,80/= na fedha kutoka kwa wahisani wa maendeleo ni 4,000,714,175/=” amesema Bwana Baragaye.
Bwana Baragaye ameeleza kuwa baada ya mapokezi, kesho Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Seregeti, tarehe 5 Julai, 2023 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, tarehe 6 Julai, 2023 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na tarehe 7 Julai, 2023 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya tarehe 8 Julai, 2023, tarehe 9 Julai, 2023 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Manispaa ya Musoma, tarehe 10 Julai, 2023 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, tarehe 11 Julai, 2023 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na hatimaye tarehe 12 Julai, 2023 Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Bwana Baragaye ameeleza kuwa baada ya kuhitimisha mbio zake katika Mkoa wa Mara, Mwenge utakabidhiwa katika Mkoa wa Mwanza tarehe 13 Julai, 2023 katika eneo la Nansio, Ukerewe.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 ni “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi wa Taifa”.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda anategemea kuwaongoza viongozi, wakimbiza mwenge, watendaji na wananchi wa Mkoa wa Mara katika mapokezi na makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa