Maandalizi ya Mkoa wa Mara kushiriki katika Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii ya “Great Lakes International Tourism Expo” (GLITE) 2020 yanayotarajiwa kufanyika katika uwanja wa CCM Kirumba, Mkoani Mwanza kuanzia tarehe 19 Juni 2020 hadi tarehe 21 Juni 2020 yanaendelea vizuri.
Akizungumza katika kikao cha pili cha wadau wa utalii wa Mkoa wa Mara kilichofanyika tarehe 17 Februari 2020 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Adam Kighoma Malima amesema Mkoa umejipanga kuonyesha vivutio vyake vya utalii, fursa za uwekezaji na kuvitangaza vivutio vipya vya utalii ambavyo havijajulikana bado.
“Sisi katika Mkoa wa Mara tunavivutio vingi sana ambavyo havijajulikana bado na havijatangazwa kabisa”. Alitoa mfano wa eneo la Nduta ambalo limo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambalo nyumbu hulitumia kuzaliana kila mwaka kati ya tarehe 5 hadi 30 Februari. Katika kipindi hiki nyumba takriban 500,000 huzaliwa katika eneo la Nduta.
Mheshimiwa Malima alisema lengo kubwa la kikao hiki cha pili ni kupata mrejesho kutoka kwa Wakurugenzi wa Manispaa, Miji na Wilaya kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo yao na fursa za uwekezaji katika vivutio vya utalii.
Akizungumza wakati akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kufungua kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bibi. Karolina Mthapula amesema maonyesho ya GLITE 2020 yanalengo la kuwakutanisha wadau wa sekta ya utalii ili kujadili maendeleo ya utalii na kutangaza vivutio vya utalii Kanda ya Ziwa.
Bibi Mthapula amesema Mkoa wa Mara utatumia fursa ya maonyesho haya kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko katika mkoa huu.
Mikoa itakayoshiriki katika maonyesho ya GLITE 2020 ni mikoa yote ya Kanda ya Ziwa yaani Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Kagera, Geita pamoja na mikoa ya Tabora na Kigoma.
Kikao cha kwanza cha wadau wa utalii Mkoa wa Mara kilifanyika tarehe 28 Januari 2020 katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa