Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani katika Mkoa wa Mara yamefanyika leo Desemba 1, 2023 katika eneo la Kisorya, Wilaya ya Bunda huku kauli mbiu ikiwa Jamii Iongoze Kutokomeza UKIMWI.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Vincent Anney amesema siku hii ni maalum kwa ajili ya kukumbushana kuwa UKIMWI bado upo tuchukue tahadhari.
Dkt. Anney ameeleza kuwa kwa sasa zana za kupambana na UKIMWI zipo na zinapatikana katika maeneo mengi mijini na vijijini na kwa sasa vipimo ili kujua hali ya afya vinatolewa bure.
Amezitaja Halmashauri zenye maambukizi makubwa kuwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma 3.8; Halmashauri ya Wilaya ya Rorya 3.6 na wastani wa Mkoa wa Mara kuwa ni 2.1.
Mhe. Dkt. Anney ameeleza kuwa kila mmoja akitimiza wajibu wake, maambukizi ya UKIMWI yatapungua na hata kuisha kabisha.
Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa Kamati za Ukimwi za Kata, Vijiji na ngazi ya Halmashauri zinafanyika na mihutasari ya vikao hivyo inawasilishwa kwenye mamlaka husika ili kupata taarifa ya masuala yaliyojiri katika vikao hivyo.
Amewashukuru wadau mbalimbali ambao wamejitoa kuusaidia Mkoa wa Mara katika mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kuimarisha utoaji wa huduma, vifaa tiba na miundombinu ya sekta ya afya.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Omari Gamuya ameeleza kuwa kwa sasa Mkoa una watu 66,436 wanaoishi na VVU na kati yao 64,315 wanatambua hali yao ya maambukizi .
Dkt. Gamuya ameeleza kuwa kati ya wote wanaojua kuhusu hali zao za maambukizi wanaume ni 20,109 na wanawake ni 44,206 wakati watoto ni 2137 na wakati watu wanaojua hali zao za maambukizi 61,099 wameanza kutumia dawa.
Ameeleza kuwa Mkoa wa Mara una jumla ya vituo vya tiba na mafunzo 174 na vituo vya tohara kinga ya kitabibu kwa wanaume 34.
Kwa mujibu wa Dkt. Gamuya, kwa mwaka 2022/2023 Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na wadau umesambaza mipira ya kiume (kondomu) 2,153,740 na kutoa elimu katika maeneo mbalimbali.
Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yamehudhuriwa na viongozi wa Wilaya ya Bunga, maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Wawakilishi kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara, wadau na wananchi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa