Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Dominicus Lusasi leo tarehe 30 Agosti, 2024 amefunga mafunzo ya wiki mbili kuhusu mifumo kwa Wakaguzi wa Ndani wa Mkoa wa Mara na kuwataka maafisa hao kuzingatia maadili ya kitaaluma.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, Bwana Lusasi amewataka Wakaguzi wa Ndani kuzingatia miiko ya Ukaguzi wa Ndani katika utendaji wao ili kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kulingana na madhumuni yake na sio vinginevyo.
“Wakaguzi wa Ndani mna majukumu makubwa sana ambayo mnawajibika nayo kama wanataaluma ikiwemo kuhakikisha taasisi ina taswira nzuri katika jamii kwa kulipa wadeni wake ikiwa ni pamoja na watumishi na wazabuni” amesema Bwana Lusasi.
Amesema, kwa sasa utekelezaji wa shughuli nyingi za Serikali unafanyika katika mifumo hivyo ni vizuri Wakaguzi wa Ndani wakaijua mifumo hiyo vizuri ili kuweza kukagua utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa ufasaha na kutoa ushauri mzuri kwa Maafisa Masuhuri wao.
Bwana Lusasi amewataka Wakaguzi wa Ndani kufuatilia mali za taasisi zao zilizoko maeneo mbalimbali na kujiridhisha na usahihi wa mali hizo kuwepo katika maeneo zilipo na kuwashauri Maafisa Masuhuri kuhusiana na taratibu za Serikali.
Bwana Lusasi amesema Serikali inaleta fedha nyingi sana katika Mikoa na Halmashauri mbalimbali lakini matumizi yake kwa sehemu kubwa sio sahihi na Wakaguzi wa Ndani ni moja kati ya watu ambao wanatakiwa kuijulisha Serikali kuhusu yanayoendelea katika maeneo yao.
“Wewe ndio jicho la taasisi yako, unatakiwa kumshauri Afisa Masuhuri kuhusu yanayoendelea katika ofisi yake kwa ukweli na uwazi, ukiona mambo hayaendi sawa na ukakaa kimya ujue wewe ni sehemu ya tatizo” amesema Bwana Lusasi.
Aidha, amewataka Wakaguzi wa Ndani kufuatilia taratibu za matumizi ya force account kwenye miradi ya maendeleo na manunuzi nje ya mfumo wa NEST na yayoyozingatia taratibu za manunuzi mambo ambayo amesema yakifanyiwa kazi vizuri yanaweza kupunguza hoja nyingi za ukaguzi wanapokuja wakaguzi wa nje.
Bwana Lusasi ameiomba TAMISEMI kutoa mafunzo zaidi ya mifumo kwa Wakaguzi wa Ndani wa Mikoa na Halmashauri hapa nchini ili kuwajengea uwezo Wakaguzi wa Ndani ikiwa ni pamoja na kuviimarisha Vitengo vya Ukaguzi wa Ndani ili viweze kukagua utekelezaji wa shughuli za Serikali na kuishauri kuhusu mapungufu yaliyomo katika taasisi mbalimbali kwa ufasaha.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Menejimenti, Usimamizi na Ufuatiliaji (MMI) Bwana Marco Maduhu amewashukuru washiriki kwa ushiriki mzuri katika mafunzo hayo, na kuwaahidi kuwa ofisi yake itaendelea kuratibu mafunzo mbalimbali kwa wakaguzi wa ndani kwa kadiri ya mahitaji.
Kwa upande wake, Mhasibu kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bwana Adolph Tikikunda ameushukuru Mkoa wa Mara kwa kuandaa mafunzo hayo kwa Wakaguzi wa Ndani na kuutaka kuendelea kuwajengea uwezo watumishi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Bwana Tikikunda amewataka Wakaguzi wa Ndani kuendelea kushirikiana kuboresha utendaji wao sehemu za kazi.
Aidha, amesema kwa sasa MMI inaandaa mafunzo ya wiki moja kuhusu ukaguzi wa miradi na mikataba ya ujenzi kwa Wakaguzi wa Ndani ili kuwawezesha kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao.
Bwana Maduhu amewataka Wakaguzi wa Ndani kuboresha utendaji wao na hususan ukaguzi ili kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kwa mujibu wa sheria, taratibu na maelekezo ya Serikali na kwa kuzingatia ubora na muda wa ukamilishaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Bwana Dismas Shadrack Waguma, Mwenyekiti wa Mafunzo hayo ameipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kuratibu mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo kuhusu mifumo mbalimbali ya Serikali.
Bwana Waguma ameuomba Mkoa kuendelea kuratibu mafunzo kama hayo mara kwa mara ili Wakaguzi wa Ndani waielewe mifumo mbalimbali ya Serikali na waweze kukagua utekelezaji wa shughuli za Serikali katika mifumo husika.
Bwana Waguma amesema washiriki wametoa maazimio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuiomba Serikali kukamilisha dirisha la ukaguzi katika Mfumo wa Manunuzi ya Umma (NEST) ili ukaguzi wa manunuzi yanayofanyika ufanyike kwenye mfumo huo.
Aidha, wamependekeza katika mfumo wa GoTHOMIS kuwa sehemu zote za mfumo huo zitumike ili kuweza kupata manufaa halisi ya mfumo huo na Mkoa uwasaidie kuratibu upatikanaji wa nywila za kuingilia katika baadhi ya mifumo ya Serikali.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yaliwahusisha Wakaguzi wa Ndani kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara, Kitengo cha Tehama na baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa