Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) leo imefanya ziara Halmashauri ya Mji wa Tarime ambapo imeipongeza Halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri wa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala na mradi wa ujenzi wa soko la kimkakati la Mji wa Tarime.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho, Makamu Mwenyekiti wa LAAC Mhe. Stanslaus Mabula amepongeza ujenzi wa jengo la utawala na usimamizi mzuri wa mradi huo uliopelekea kukamilisha mradi na kubakisha fedha.
“Kazi iliyofanyika hapa kwenye jengo hili ni kubwa sana na mmefanikiwa kujenga uzio kuzunguka ofisi na kibanda cha mlinzi kazi ambazo hazikuwa sehemu ya mradi huu na kubakiza shilingi milioni 82 katika utekelezaji wa mradi huu” amesema Mhe. Mabula.
Hata hivyo, ameitaka Halmashauri hiyo kujibu hoja za ukaguzi zilizoibuliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kuhusu malipo ya awali aliyopewa mkandarasi wa jengo la utawala, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), shilingi 258,872,578.56.
Mhe. Mabula ameitaka Halmashauri hiyo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za manunuzi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na amempongeza Mhandisi wa Halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.
Mhe. Mabula amesema kuwa jengo la Halmashauri hiyo lina ramani nzuri ambazo hazitumiki kwa katika kujenga majengo ya utawala ya Halmashauri ikilinganishwa na jengo la Halmshauri ya Wilaya ya Tarime lenye ramani inayotumika kwa sasa ambayo amesema sio nzuri kama ramani za awali.
Akizungumzia ujenzi wa soko, Mhe. Mabula ameitaka Halmashauri kuhakikisha inarejesha malipo ya awali aliyopewa mkandarasi wa mradi huo Mohamed Builders shilingi bilioni 1.27 kabla ya mradi haujakamilika na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu malipo ya mkandarasi wa jengo la utawala, Mhandisi wa Halmashauri hiyo Eng. Daudi Bucheye ameeleza kuwa ni kweli kulikuwa na mapungufu katika malipo ya awali aliyolipwa TBA, hata hivyo baada ya kukaa pamoja na mkandarasi imebainika kuwa katika milioni 500 alizopewa tayari shilingi 374,340,530.25 zimerejeshwa.
“Shilingi 125,659,469.75 bado hazijareshwa kwa malipo ya hati ya nane ya tarehe 22 Septemba, 2023 na Halmashauri bado inayo fedha ya zuio ya shilingi 110,430,456.42 ambayo kama itachukuliwa, mkandarasi bado atakuwa anadaiwa shilingi 15,229,001.33” amesema Mhandisi Bucheye.
Aidha, Mhandisi Bucheye ameieleza Kamati hiyo kuwa Halmashauri imeanza kutumia kanuni mpya ya kumkata mkandarasi anayejenga soko fedha alizopewa awali na kwa kutumia kanuni hiyo mradi utakapofikia asilimia 80 ya malipo, mkandarasi atakuwa ameshakatwa fedha yote aliyolipwa awali ili Halmashauri isibakie na deni.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Bibi Fortunata Matinde ameeleza kuwa TAMISEMI imepokea maelekezo ya Kamati na itafuatilia utekelezaji wake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Bibi Matinde ameihakikishia Kamati hiyo kuwa TAMISEMI itahakikisha Halmashauri inazingatia masuala ya kisheria katika utekelezaji miradi mbalimbali kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Ameeleza kuwa suala la mabadiliko ya ramani za majengo ya utawala ya Halmashauri Ofisi ya Rais TAMISEMI italifanyiakazi kwa kuzingatia maoni ya Kamati ili kupata ramani nzuri zaidi zenye ubora katika majengo ya Halmashauri hapa nchini.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Mkoa wa Mara umeyapokea maelekezo yote ya Kamati na utasimamia utekelezaji wa maagizo yote kwa wakati.
Bwana Kusaya amesema Mkoa pia utasimamia ukamilishaji wa mradi wa soko la kimkakati la Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa ubora na wakati kwa mujibu wa mkataba ili wananchi waanze kupata huduma.
Ziara hiyo imehudhuriwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, maafisa kutoka TAMISEMI, Ofisi ya Bunge, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kadhalika.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa