Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) leo imefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kuelezea kuridhishwa kwake na mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Nyasaricho.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho, Makamu Mwenyekiti wa LAAC Mhe. Stanslaus Mabula ambaye ameongoza msafara huo ameeleza kuwa ujenzi wa mradi huo umesimamiwa vizuri na shule hiyo imewekwa katika mazingira mazuri na ya usafi.
“Ninampongeza Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyasaricho kwa kuweka mazingira vizuri na katika hali ya usafi na ninamuombea aendelee kuwepo katika shule hii kwa maana anastahili” amesema Mhe. Mabula.
Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kuwataka mameneja wa Wilaya wa TANESCO na RUWASA kuhakikisha kuwa huduma za maji na umeme zinafika katika Shule ya Sekondari ya Nyasaricho.
Akizungumzia kuhusu jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mhe. Mabula ametoa miezi mitatu kwa mkandarasi wa jengo hilo SUMA JKT kurudia rangi baadhi ya sehemu na kufanya usafi wa rangi zilizomwagika maeneo mbalimbali wakati wa umaliziaji wa jengo hilo.
Mhe. Mabula ameiagiza Halmashauri hiyo kununua samani za ofisi zinazendana na jengo hilo haraka iwezekanavyo ili watumishi waweze kufanya kazi katika mazingira mazuri.
Akizungumzia kuhusu samani za jengo la ofisi, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bwana Solomon Shati ameeleza kuwa tayari Halmashauri imetenga fedha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa samani katika mwaka wa fedha 2023/2024.
“Tayari matangazo ya kutafuta wazabuni wa kutengeneza samani hizo yapo kwenye mfumo wa ununuzi wa NEST, na taratibu za manunuzi zikikamilika, kutakuwa na samani mpya katika ofisi zote za jengo hilo” amesema Bwana Shati.
Bwana Shati ameahidi kumsimamia mkandarasi kukamilisha shughuli zilizobakia pamoja na kufanya usafi wa jengo hilo ndani ya muda mfupi kabla ya malipo yao ya mwisho kwa ajili ya kazi hayajafanyika.
Aidha, wabunge mbalimbali wamechangia kuhusu ziara hiyo wamepongeza ujenzi na usimamizi wa shule hiyo huku Mbunge wa Jimbo Serengeti Mhe. Amsabi Mrimi akiishauri Halmashauri kuongeza eneo la shule hiyo na kupanda miti ya kivuli kuzunguka shule hiyo ili wanafunzi wapate eneo zuri kwa ajili ya kujisomea.
Baadhi ya wabunge pia wameiomba Halmashauri kuhakikisha inaweka umeme katika shule hiyo ili watumishi na wanafunzi waweze kukaa maeneo mazuri na kuweza kujisomea kiurahisi.
Kamati hiyo leo imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Shule ya Sekondari ya Nyasarisho katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kesho Kamati ya LAAC itatembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la utawala na soko la kimkakati katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Shule ya Sekondari ya Nyasaricho imejengwa baada ya Halmashauri kupokea shilingi bilioni 1 wa kujenga shule ya bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kutwa kidato cha kwanza hadi cha nne na wanafunzi wa bweni kidato cha tano na sita ambapo Halmashauri pia imeongezea shilingi milioni 600,000 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa shule hiyo.
Ziara hiyo imehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Bwana Wilson Charles Mahera, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, maafisa kutoka TAMISEMI, Ofisi ya Bunge, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kadhalika.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa