Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) leo imefanya ziara katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma ambapo imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Rwamlimi na Shule ya Sekondari ya Kigera Mwiyale na kuipongeza Manispaa hiyo kwa usimamizi mzuri wa mradi.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho, Makamu Mwenyekiti wa LAAC Mhe. Stanslaus Mabula ambaye ameongoza msafara huo, ameipongeza Manispaa ya Musoma kwa usimamizi mzuri wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Rwamlimi.
“Ujenzi wa Shule ya Sekondari (Kigera Mwayale) ukamilike mapema iwezekanavyo, madarasa yawekewe vigae na gharama za nyongeza katika majengo yanayohitaji ukamilishaji ziendane na uhalisia kulingana na kazi iliyobakia” amesema Mhe. Mabula.
Aidha, Mhe. Mabula ameitaka Manispaa ya Musoma kujibu hoja za ukaguzi zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) katika Mwaka wa fedha 2021/2022 na kuwasilisha majibu hayo kwa Mkaguzi kabla ya Septemba, 2024.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Bwana Bosco Ndunguru ametoa ufafanuzi kuhusiana na hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wabunge katika kikao cha majumuisho.
Bwana Ndunguru ameeleza kuwa fedha za Shule hiyo zilikuja kwa ajili ya Kata ya Kwangwa ambayo awali kabla ya kugawanywa ilikuwa ni kata moja na Kigera na Uongozi wa Manispaa ulibadilisha matumizi ya fedha hizo ili kujenga shule Kata ya Kigera ambayo ilikuwa haina Shule ya Sekondari.
“Maamuzi haya yamesaidia sana kupunguza idadi ya wanafunzi katika shule ya Kwangwa na kuwapunguzia umbali wanafunzi wa Kigera kwenda Kwangwa na badala yake kwa sasa wanasoma katika Shule ya Sekondari ya Kigera Mwiyale” amesema Bwana Ndunguru.
Bwana Ndunguru ameeleza kuwa Halmashauri kupitia mapato ya ndani imelipa fidia kwa wananchi milioni 82 ili kuweza kupata eneo la kujenga shule hiyo na imetenga fedha shilingi milioni 200 katika bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa nane katika shule hiyo.
Aidha, Bwana Ndunguru amesema Manispaa imeomba shilingi milioni 153 kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo ya shule hiyo baada ya fedha zilizopokelewa shilingi milioni 470 kuisha na baadhi ya majengo yakiwa hayajakamilika.
Awali, wakitoa michango yao, baadhi ya wabunge mbali na kupongeza ujenzi wa miradi hiyo waliomba ufafanuzi kuhusiana na kwa nini fedha ilibadilishiwa kata ya kujenga mradi kutoka Kata ya Kwangwa hadi Kata ya Kigera na mchango wa Halmashauri katika ujenzi wa mradi wa Shule ya Sekondari ya Kigera Mwiyale.
Ziara hiyo imehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Meya wa Manispaa ya Musoma, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Musoma, maafisa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Manispaa ya Musoma.
Kesho, Kamati ya LAAC itatembelea na kukagua miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama ambapo itatembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kamugegi na Hospitali ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa