Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) leo imefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambapo imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti inayoendelea kujengwa katika eneo la Kibeho, katika Mji wa Mugumu.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho, Makamu Mwenyekiti wa LAAC Mhe. Stanslaus Mabula ambaye ameongoza msafara huo, amepongeza Halmashauri hiyo kwa kazi nzuri iliyofanyika katika ujenzi wa Hospitali hiyo.
“Fundi aliyetengeneza milango ya majengo mbalimbali ya hospitali amefanyakazi nzuri sana na hospitali ina mazingira masafi sana yanayostahili pongezi za Kamati” amesema Mhe. Mabula.
Mhe. Mabula ameitaka Halmashauri hiyo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za manunuzi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kujibu hoja 10 za ukaguzi zilizoibuliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kuhusuiana na mradi huo ambazo Halmashauri haijaweza kuzijibu mpaka sasa.
Aidha, Mhe. Mabula ambaye ni Mbunge wa Nyamagana, ameitaka Halmashauri hiyo kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu matumizi ya fedha za Halmashauri.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Mkoa wa Mara umeyapokea maelekezo yote ya Kamati kwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na utasimamia utekelezaji wa maagizo yote kwa wakati.
Bwana Kusaya amesema Mkoa pia utasimamia ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ili kuimarisha mapato ya Halmashauri hiyo na kuboresha huduma kwa wananchi na kuwasimamia watumishi katika utendaji kazi wao.
“Tunataka kuona Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ikibadilika na kuwa Halmashauri ya mfano katika Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla katika ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa matumizi ya fedha zake” amesema Bwana Kusaya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bwana Afrah Hassan ametoa ufafanuzi wa baadhi ya maswali aliyoulizwa na Kamati ya LAAC, ameeleza kuwa tayari Halmashauri imejibu hoja zote 10 za CAG na kuziwakilisha katika ofisi za CAG Mkoa wa Mara kwa ukaguzi.
Bwana Hassan ameeleza kuwa kutokana na changamoto ya Uviko 19 na mapato ya Halmashauari hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa yanategemea utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kwa mwaka wa fedha 2019/2020-2021/2022 Halmashauri hiyo haikupata mapato ya kutosha.
Bwana Hassan ameeleza kuwa hii ilitokana na makampuni zaidi ya 200 kushindwa kujiendesha na kufunga biashara zao katika Wilaya ya Serengeti katika kipindi hicho na hivyo kuathiri mapato ya Halmashauri hiyo.
Hata hivyo Bwana Hassan ameihakikishia Kamati hiyo kuwa kwa mwaka 2022/2123 Halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 4.4 ambayo ni sawa na asilimia 114 mapato ya shilingi bilioni 3.9 zilizokuwa zimepangwa katika bajeti ya mwaka huo.
Bwana Hassan amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri hiyo inategemea kukusanya zaidi na kwa hatua za ukusanyaji wa mapato zilipofikia wanategemea kuvuka lengo kama mambo yataenda kama ilivyo sasa.
Ziara hiyo imehudhuriwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, maafisa kutoka TAMISEMI, Ofisi ya Bunge, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kadhalika.
Kesho, Kamati ya LAAC itatembelea na kukagua miradi katika Manispaa ya Musoma ambapo itatembelea na kukagua Zahanati ya Rwamlimi na Shule ya Sekondari ya Kigera.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa