Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo ameongoza kikao tathmini na mipango ya utekelezaji wa mradi wa Kizazi Hodari Mkoa wa Mara killichofanyika katika ukumbi wa uwekezaji na kuzitaka Halmashauri kutoa ushirikiano kwa taasisi zinazotekeleza mradi huo.
“Halmashauri na watekelezaji wa mradi huu mkishirikiana kwa ukaribu, malengo ya mradi yatafikiwa kiurahisi na Halmashauri mtagundua mapema kuhusu mambo mazuri na mapungufu kama yapo katika utekelezaji wa mradi huu” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amezitaka Halmashauri kutoa ofisi kwa ajili ya taasisi ya Rafiki SDO ili maafisa wa taasisi hiyo wapate sehemu ya kufanyia kazi na kuwashirikisha wadau wanapofanya ufuatiliaji wa shughuli za Halmashauri ili taasisi hizo ziweze kutumia kwa pamoja magari yaliyopo.
Bwana Kusaya amezishukuru taasisi zinazotekeleza mradi huo kwa ufadhili wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID) na kuzitaka taasisi hizo kuangalia namna ambavyo zinaweza kuzisaidia Halmashauri mbili za Mkoa wa Mara ambazo hazimo kwenye mradi huo kunufaika na mradi huo.
Katibu Tawala amepongeza mradi huo kwa kupata mafanikio makubwa ambapo idadi ya watu waliopangwa kunufaika imeongezeka na utekelezaji wa mradi kwa mwaka 2024 umewafikia asilimia 120 ya walengwa waliopangwa kufikiwa na mradi husika.
Bwana Kusaya amewataka wataalamu wote wanaohusika na mradi huo kuendelea kuwa wabunifu katika utekelezaji wa mradi huo na kuhakikisha Mkoa wa Mara unafanya vizuri ili kuwalinda watoto na kutimiza malengo ya mradi huu.
Kwa upande wake, Bwana Haruni Haruni mtaalamu wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na lishe Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) amezipongeza taasisi za Rafiki SDO, Amref na ELCT kwa kazi nzuri wanayoifanya katika utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Mara.
Bwana Haruni amewataka maafisa wa Serikali kuonyesha ushirikiano kwa wadau wote wanaofanyanao kazi na kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kufanya utambuzi wa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ili kuwaunganisha na huduma.
Aidha, Bwana Haruni amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuongeza fedha kwenye maeneo ambayo mashirika hayo hayajayafikia ili kufanya utekelezaji wa malengo ya mradi huo kufikiwa na kuleta tija kwa watoto wanaonufaika na mradi huo.
Bwana Haruni amewataka Halmashauri kupitia Idara za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kuwashirikisha wadau hao katika kuweka mipango na bajeti za mwaka ili kuweza kubaini maeneo ya kipaumbele na mapungufu katika bajeti yanayohitaji Serikali kuingilia kati.
Bwana Haruni ameutaka Mkoa wa Mara kujihadhari na magonjwa ya mlipuko na hususan kipindupindu ambacho kipo katika mikoa ya jirani kwa kuendelea kutoa elimu ya afya na kuwahamasisha wananchi kuhusiana na matumizi ya vyoo bora.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi Hodari Kanda ya Kaskazini Mashariki, KKKT Makao Makuu Dkt. Godson Maro amesema mradi utaangalia uwezekano wa kutoa mafunzo kwa Maafisa Ustawi wa Jamii kuhusu ujazaji wa taarifa katika mfumo kuhusiana na mradi huo.
“Ni matumaini yetu kuwa Maafisa Ustawi wa Jamii wakiwezeshwa watatekeleza makujukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kujaza taarifa sahihi kwenye mfumo” amesema Dkt. Maro.
Dkt. Maro amezishukuru Halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa ushirikiano uliopo katika utekelezaji wa mradi wa Kizazi Hodari pamoja na taasisi zote zinazohusika na kuongeza kuwa anaunga mkono suala la kuwa na usimamizi shirikishi.
Dkt. Maro amezitaka Halmashauri kununua makabati na vitendea kazi kwa ajili ya ofisi za kata ili maafisa wapate sehemu ya kuhifadhia taarifa za mashauri ya watoto.
Kikao hiki kimehudhuriwa na Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Halmashauri saba zinazotekeleza mradi huo, viongozi wa dini na taasisi nyingine zinazotekeleza mradi huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa