Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo tarehe 19 Julai, 2024 ameongoza kikao cha tathmini ya Programmu Jumuishi ya MAlezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto na kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuongeza bajeti ya Vitengo vya Ustawi wa Jamii ili viweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Bwana Kusaya amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga magari kwa ajili ya Maafisa Ustawi wa Jamii ili waweze kufuatilia kwa ukaribu changamoto za wananchi na hususan watoto katika maeneo mbalimbali wanayofanyia kazi.
“Tukiviwezesha Vitengo vya Ustawi wa Jamii tutapunguza wananchi wenye kero wanaokuja kuwaona viongozi kwa kero mbalimbali, kwa sababu Maafisa Ustawi wa Jamii watazipunguza baadhi ya kero hizo” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya pia amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha programu hii inazinduliwa katika ngazi za Kata, Mtaa na Vijiji katika Halmashauri zote na kuipongeza Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kufanikiwa kuzindua programu hiyo katika Kata zake zote nane za Halmashauri hiyo.
Bwana Kusaya amesema programu hii inawaleta pamoja wadau wa maendeleo wa sekta mbalimbali ili waweze kufanyakazi kwa ushirikiano katika kuhakikisha watoto wenye umri wa miaka 0-8 wanapata huduma za malezi jumuishi, wanastawi na kufikia hatua za ukuaji timilifu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara amesema programu hii inatekelezwa katika vipengele vikuu vitano ambavyo ni lishe toshelevu, malezi yenye mwitikio, ulinzi na usalama, afya bora na fursa za ujifunzaji wa awali.
Kwa upande wake, Bibi Mary Shillah Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum ameupongeza Mkoa wa Mara kwa uwakilishi mzuri wa maafisa wa Serikali na wadau wengi kujitokeza katika kikao hicho.
Bibi Shillah ameeleza kuwa Serikali imeamua kufuatilia watoto katika umri wa miaka 0-8 kwa sababu wataka wadau wengine waongezeke kama vile Benki ambazo zina akaunti maalum za watoto,
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mara Bi. Elizabeth Mahinya amewaomba Wakurugenzi wa Halmashauri kuongeza bajeti ya Vitengo vya Ustawi wa Jamii ili vitengo hivyo viweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kuihudumia jamii.
Bi. Mahinya amesema watendaji waliopo wanaweza kutekeleza majukumu yao vizuri lakini wanakwamishwa na bajeti zinazotengwa katika vitengo hivyo katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha, Bi. Mahinya amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kufanyakazi kwa ushirikiano ili kwa umoja wao waweze kupata matokeo makubwa katika kuwahudumia wananchi.
Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto ilianza kutekelezwa mwaka 2021/2022- 2025/2026 na ilizinduliwa rasmi tarehe 13 Desemba, 2021 katika Jiji la Dodoma na Mhe. Doroth Gwajima Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Maafisa Ustawi wa Jamii na wadau mbalimbali wanaoshirikiana na Halmashauri katika kutekeleza programu hiyo katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa