Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Kusaya amezungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee ambayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika katika Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara tarehe 13-15 Juni, 2024.
Bwana Kusaya amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kuanza kufanyika tarehe 13 Juni, 2024 kwa wazee kushiriki michezo mbalimbali itakayofanyika katika Shule ya Sekondari ya Bunda na zoezi la kupima afya litakalofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Miembeni.
“Zoezi la kupima afya kwa wazee wote litakuwa bure na litafanywa na wataalamu wetu wa afya waliopo katika Mkoa wa Mara na wazee watapatiwa matibabu katika viwanja hivyo” amesema Bwana Kusaya.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tarehe 14 Juni, 2024 kutakuwa na kongamano litakalojadili masuala mbalimbali ya Wazee ambalo litafanyika Chuo cha Ualimu Bunda na kufuatiwa na ziara ya Wazee nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Bwana Kusaya amesema kilele cha maadhimisho hayo itakuwa ni tarehe 15 Juni, 2024 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wananwake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb.).
Bwana Kusaya amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni: Utu, Usalama na Ustawi ni nyenzo ya Kutokomeza vitendo vya Ukatili dhidi ya Wazee na kuwaomba wananchi wote kujitokeza kushiriki katika matukio mbalimbali ya maadhimisho haya.
Bwana Kusaya amezungumza na Waandishi wa Habari baada ya kuhitimisha kikao cha tatu cha maandalizi kilichowahusisha viongozi, watumishi wa umma na wadau mbalimbali kilichofanyika katika ukumbi wa Herieth uliopo katika Mji wa Bunda.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa