Katibu Tawala Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya leo tarehe 25 Julai, 2025 amepokea jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama baada ya Mkandarasi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kukamilisha ujenzi wa jengo hilo.
Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya jengo hilo, Ndugu Kusaya amesema ameridhika na hatua iliyofikia ya ujenzi wa jengo hilo na kwa sasa Mkuu wa Wilaya ya Butiama anaweza kuhamia katika jengo hilo.
“Nimeridhika na ujenzi wa jengo hili, kwa sasa Mkuu wa Wilaya ya Butiama anaweza kuhamia katika jengo hili huku akisubiria samani kwa ajili ya ofisi hiyo ambazo zitanunuliwa hivi karibuni” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amemuagiza Meneja wa TBA Mkoa wa Mara kufanyiakazi marekebisho madogo madogo yaliyobainika katika jengo hilo haraka iwezekanavyo ili Mkuu wa Wilaya atakapohamia jengo liwe vizuri.
Aidha, ameitaka TBA kutoa mafunzo kuhusu mifumo mbalimbali iliyofungwa katika jengo hilo kwa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama ili waweze kuitumia kwa usahihi mifumo hiyo.
Bwana Kusaya amemtaka Katibu Tawala wa Wilaya kuandaa ulinzi wa jengo hilo baada ya mkandarasi kuondoka katika jengo hilo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu Mhandisi Richard Moshi amemshukuru Katibu Tawala wa Mkoa kwa kupokea jengo hilo na kumuomba Mkandarasi kukamilisha marekebisho madogo madogo yaliyobainishwa kabla ya Mkuu wa Wilaya hajahamia katika jengo hilo.
“Haitapendeza Mhe. Mkuu wa Wilaya yupo ofisini harafu fundi anapita kurekebisha vitu katika jengo hili” amesema Mhandisi Moshi.
Kwa upande wake, Meneja wa TBA Mkoa wa Mara Arch. Jeje Nicolaus Jeje amesema marekebisho yote yaliyobainika katika ukaguzi huo yatafanyiwa kazi hadi tarehe 30 Agosti, 2025 yatakuwa yamekamilika.
“Kwa sababu marekebisho ni kidogo, ninaahidi hadi tarehe 30 Agosti, 2025 jengo hili litakuwa tayari kwa ajili ya matumizi ya Mhe. Mkuu wa Wilaya” amesema Arch. Jeje.
Arch. Jeje amesema watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya watapatiwa mafunzo ya namna ya kutumia mifumo mbalimbali iliyofungwa katika jengo la ofisi hiyo mapema iwezekanavyo ili kuwawezesha kuitumia vizuri mifumo hiyo.
Wakati huo huo, Katibu Tawala wa Mkoa ametembelea Wakala wa Umeme na Ufundi (TEMESA) na Gereji ya Jassie zilizopo Manispaa ya Musoma kwa ajili ya kukagua maendeleo ya matengenezo ya magari ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara yanayotengenezwa katika gereji hizo.
Katika ziara hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Mkoa wa Mara na watumishi wa TBA na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa