Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo tarehe 14 Mei, 2024 amefanya ziara katika Wilaya ya Butiama ambapo amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT), Butiama.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Bwana Kusaya ameitaka Menejimenti ya Chuo cha MJNUAT na Mshauri welekezi wa mradi huo kusimamia kikamilifu na kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa ubora.
“Huu mradi unapaswa kukamilika mapema kulingana na mikataba yake ili watu waweze kuanza kupata huduma za elimu kwa wakati na utekelezaji wake uzingatie viwango vya ubora vya majengo haya” amesema Bwana Kusaya.
Majengo yanayojengwa katika mradi huo ni Chuo cha Kilimo, Skuli ya Kilimo, usindikaji na Teknolojia, Skuli ya Uhandisi na Teknolojia ya Nishati na Madini, jengo la utawala, barabara na njia za kupita, mabweni, cafeteria, maabara na kalakana za uhandisi na kilimo kwa gharama ya shilingi bilioni 102.5.
Mradi huo unaotekelezwa na wakandarasi mbalimbali unategemewa kutekelezwa kwa muda wa miezi 18 kuanzia Novemba, 2023 na unapaswa kukamilika ifikapo Mei, 2025 na kwa sasa umefikia wastani wa asilimia 18. 5 ya utekelezaji wake.
MJNUAT ni moja kati ya taasisi 22 za Elimu ya Juu nchini Tanzania zilizonufaika na mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Mradi wa HEET una lengo la kuboresha miundombinu na mifumo ya kitaasisi ya Vyuo vya elimu ya Juu hapa nchini na unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021-2026.
Katika ziara hiyo, Katibu Tawala aliambatana na baadhi ya maofisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Menejimenti ya Chuo cha MJNUAT.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa