Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo ameongoza kikao cha wadau wa Mkoa wa Mara katika utambulisho wa wataalamu wa mazingira kutoka Harmonic Biosphere Company Limited watakaofanya tathmini ya athari ya mazingira na kijamii katika upanuzi wa Mgodi wa Barrick North Mara kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika kikao hicho, Bwana Kusaya ameutaka Mgodi wa Barrick North Mara kuongeza jitihada zaidi katika kuboresha mawasiliano na mahusiano na Serikali, wananchi na wadau mbalimbali wanaouzunguka mgodi huo uliopo katika eneo la Nyamongo, Wilaya ya Tarime.
“Kaeni karibu na wananchi na kuwasikiliza mawazo yao, mahusiano ya mgodi na wananchi na wadau wengine yakiimarishwa, wananchi wanaouzunguka mgodi na wadau wengine watakuwa na imani na mgodi na watawasaidia katika ulinzi na hata shughuli zenu zitafanyika vizuri” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amesema kuwa Serikali ya Mkoa wa Mara inatamani kuona shughuli ya tathmini na zoezi la kuwalipa fidia fidia wananchi linafanyika vizuri bila kuleta kero kwa wananchi wa eneo hilo watakaotakiwa kuhama kupisha upanuzi wa shughuli za mgodi.
Bwana Kusaya amesema kwa sasa Mkoa utasimamia kuhakikisha kuwa miradi ya CSR inayotolewa Noth Mara inafanyika kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu ili kutekeleza miradi ambayo itawaletea wananchi maendeleo endelevu na sio kutekeleza miradi ambayo haina manufaa kwa jamii.
Aidha, ameutaka mgodi huo kuwapeleka wadau hao katika eneo ambalo upanuzi unatarajiwa kufanyika na maeneo ya wananchi wanaotarajiwa kuhamishwa ili kuona hali halisi itakayowasaidia kutoa ushauri baada ya kuona hali halisi ya eneo husika.
Kwa upande wake, Bi. Sarah Cyprian Mtaalamu wa Mazingira kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara ameeleza kuwa upanuzi huo utahusisha shimo la wazi la Nyabilama ambalo kwa sasa lina urefu wa mita 345 kwenda chini na mradi huo unalenga kuliongeza kufikia mita 370 kwenda chini.
Maeneo yatakayoathirika zaidi ni mashariki na magharibi ya shimo la sasa ambako upande wa mashariki kuna mtambo wa kusagia mawe utakaohamishwa na upande wa magharibi kuna makazi ya watu ambao pia watalipwa fidia ili kupisha uendelezaji wa eneo hilo.
Bi. Sarah amesema kwa mujibu wa taratibu za uchimbaji wa madini kimataifa zitazingatiwa na kati ya shimo hilo na makazi ya watu kutakuwa na eneo la wazi lenye mita 200 ili kupunguza athari za uchimbaji wa madini kwa binadamu.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa mgodi huo Bwana Amos Maganga ameeleza kuwa kwa sasa zoezi la kufanya uthamamini katika eneo hilo limefanyika ambapo jumla ya watu 953 ambao kati yao wamiliki ni 724 na wengine ni wapangaji watatakiwa kulipwa fidia na kuhamishwa katika eneo hilo.
Bwana Maganga amesema vijiji vitakavyofikiwa katika upanuzi huo ni Nyabichune, Mjini Kati na Matongo vilivyopo katika Kata ya Matongo, Wilaya ya Tarime na mpaka sasa zoezi la uthamini limeridhiwa na wanufaika wote na mgodi unaendelea na mazungumzo na watu 10 ambao hawajaridhika na uthamini uliofanywa katika eneo hilo ili waweze kuridhia.
Bwana Maganga amesema kwa maboresho ya fidia yanayofanyika sasa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na bei ya soko wanategemea hakutakuwa na migogoro mingi katika ulipaji wa fidia kwa wananchi na wamejiandaa kufanya majadiliano katika kila hatua kama kutakuwa na uhitaji wa kufanya hivyo.
Kwa upande wao, wataalamu kutoka Harmonic Biosphere Company Limited wameomba ushirikiano katika utekelezaji wa zaozi la kufanya tathmini ya athari ya kimazingira katika utekelezaji wa mradi huo ili waweze kukamilisha kazi yao kwa muda uliopangwa.
Kikao hicho kiliwahusisha baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa wa Mara, Menejimenti na baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, wataalamu kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mara, RUWASA Mkoa wa Mara na kadhalika.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa