Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 11 Julai, 2024 imekagua miradi itakayotembelewa na Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 katika Wilaya za Serengeti na Tarime.
Kamati ikiwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imekagua ujenzi wa soko la Kijiji cha Makundusi linalojengwa kwa mapato ya Kijiji hicho na Barabara ya Parknyigoti hadi Nichoka pamoja na ujenzi wa daraja.
Kamati ikiwa katika Halmashauri hiyo, imepokea taarifa ya miradi yote itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru na taarifa ya utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa na Kamati ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Kamati ilikagua mradi wa jengo la kitega uchumi la Nyamongo Plaza linalomilikiwa na Bwana Josephati Mwita pamoja na mradi wa maji wa Nyangoto ambao ulitekelezwa kwa ufadhiri wa Mgodi wa Barrick North Mara na ulizinduliwa na Mwenge wa Uhuru na kwa mwaka huu utaenda kuangalia uendelezaji wake.
Katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, Kamati ilikagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Kede ambayo imejengwa kwa fedha za Serikali, mchango wa wananchi na mchango wa Halmashauri ya Mji wa Tarime na Daraja la Kinyambi katika mto Moi linalojengwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
Ikiwa katika Wilaya ya Tarime, Kamati imepokea taarifa ya miradi yote itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru na taarifa ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Kamati ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Kamati iliziagiza Halmashauri hizo kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na kuandaa hamasa kubwa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri hizo.
Kamati ya Usalama ya Mkoa iliambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti na Wilaya ya Tarime, wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri za Tarime DC, Tarime TC na Serengeti DC.
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kupokelewa katika Mkoa wa Mara tarehe 26 Julai, 2024 ukitokea Mkoa wa Arusha na utakimbizwa katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara hadi tarehe 4 Agosti, 2024 utakapokabidhiwa katika Mkoa wa Simiyu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa