Mradi wa upanuzi wa Zahanati ya Kijiji cha Genkuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime uliotengewa zaidi ya milioni 700 haujakamilika huku fedha zikitumika kununua vifaa vingi vilivyobakia stoo.
Hayo yamebainika leo tarehe 13 Agosti 2021 katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mara aliyoifanya katika mradi huo unaojengwa kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii zilizotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara mwaka 2018.
Kufuatia tatizo hilo Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameagiza kukamatwa kwa watu wote waliohusika kwa namna moja au nyingine na mradi huo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
“Nawaagiza Polisi na TAKUKURU kukamata watu wote wanaohusika na mradi huu ili waweze kuzirejesha fedha zilizotumika vibaya katika mradi huu” alisema Mheshimiwa Hapi.
Akikagua mradi huo Mheshimiwa Hapi ameshuhudia vifaa vingi vikiwa vipo stoo na vingine kama vile matofali, karatasi za kuzuia maji, vigae, nondo na mabati vikiwa vimebakia kwa wingi lakini havihitajiki tena.
Mheshimiwa Hapi amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuchunguza uhalili wa matumizi ya fedha nyingine ambazo zililetwa katika kijiji hicho.
Fedha hizo ni shilingi milioni 100 zinazodaiwa kupelekwa kijiji kingine; milioni 37 zinazodaiwa kulipa mawakili waliosimamia kesi; milioni 15 zinazodaiwa kulipa wadhamini wa kesi; huku milioni 18 zikilipwa viongozi wa kijiji waliokuwa wanahudhuria kesi Mahakama Kuu, Mwanza.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Genkuru Bwana Gichovu Chacha ameeleza kuwa vifaa vilivyonunuliwa vilitokana na maelekezo waliyopewa na Afisa Mununuzi na Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambao ndio walikuwa wataalamu katika utekelezaji wa mradi huo.
Bwana Chacha ameyataja majengo yaliyojengwa katika mradi huo kuwa ni cliniki ya Baba, Mama na Mtoto (RCH), jengo la Mama na Mtoto, jengo la upasuaji, mochwari, maabara na nyumba moja pacha ya watumishi, choo cha matundu manne.
Mtendaji huyo ameeleza kuwa hamna jengo hata moja lililokamilika baada ya fedha nyingi kutumika kununua vifaa ambavyo havihitajiki tena katika mradi huo huku fedha za kukamilisha mradi huo zikiwa hamna.
Wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wananchi wa kijiji hicho wameeleza kuwa huu ni mwaka wa kumi uongozi wa kijiji chao hauwapi taarifa za mapato na matumizi ya kijiji chao.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa