Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Lt. Josephine Paul Mwambashi amewapongeza wanachi wa kijiji cha Balata kwa kujenga shule ya sekondari tarajali ili kupunguza umbali wa wanafunzi kwenda kufuata masomo katika shule iliyokuwa jirani.
Lt. Mwambashi ametoa pongezi hizo wakati wa kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa shule hiyo ambapo madarasa manne na ofisi moja ya walimu yapo katika hatua mbalimbali katika ujenzi wake.
“Ninawapongeza sana wananchi kwa kuona umuhimu wa elimu ya watoto wenu na kuwapunguzia umbali wa kutembea kufuata masomo” alisema Mwambashi.
Lt. Mwambashi ameeleza kuwa kitendo cha wananchi wa Kijiji cha Balata ni mfano wa kuigwa hata na wananchi wa sehemu nyingine ili kuweza kujiletea maendeleo yao kwa haraka.
Hata hivyo mradi huo ulikuwa na mapungufu kadhaa yaliyosababishwa na wataalamu waliokuwa wanausimamia kutokuweka vizuri nyaraka za mradi na kutokupima vifaa vilivyotumika katika ujenzi wa shule hiyo.
“Mwenge unaweka jiwe la msingi lakini naagiza nipate maelezo kutoka kwa Mhandisi kwa nini kupima vifaa ni gharama na vilelezo vya nyaraka zote ambazo hatujapata hapa hadi saa 12 jioni ya leo” alisema Mwambashi.
Katika kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kijiji cha Balata, Mbunge wa Tarime Vijijini Mheshimiwa Mwita Waitara ameahidi kutoa shilingi milioni kumi kutoka katika mfuko wa jimbo ili kuongeza nguvu katika juhudi za wananchi hao.
“Mimi ninawapongeza sana kwa juhudi zenu, mmefanya jambo kubwa sana kwa maendeleo ya watoto wenu na Taifa kwa ujumla, mimi nitawaunga mkono kwa kutoa shilingi milioni 10 kutoka katika mfuko wa jimbo ili ziweze kusaidia” alisema Mheshimiwa Waitara.
Mheshimiwa Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi aliungana na msafara wa Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Wilaya ya Tarime.
Aidha mwenge wa uhuru umeweka jiwe la msingi katika barabara ya Kewanja hadi Nyangoto katika eneo la Nyamongo yenye urefu wa kilomita 2.93; umetembelea mradi wa vitalu vya miche ya kahawa katika eneo la Nyamwaga; umezindua kituo cha mafuta cha PKM na mradi wa maji katika eneo la Gamasara.
Mwenge wa Uhuru pia umezindua nyumba tatu za watumishi na kutembelea mradi wa kukusanya mapato kielectroniki katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime; na kutembelea mradi wa barabara ya kilomita moja iliyozinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2019.
Mwenge wa Uhuru kwa leo unafanya mkesha katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Tarime na kesho utakabidhiwa katika Wilaya ya Rorya kuendelea na mbio zake.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizinduliwa tarehe 17 Mei 2021 katika Mkoa wa Kusini Unguja na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Wiki ya Vijana Kitaifa 2021 itafanyika mkoani Geita tarehe 14 Oktoba 2021.
Katika Mkoa wa Mara Mwenge wa Uhuru unakimbizwa kuanzia tarehe 22 Juni 2021 hadi tarehe 27 Juni 2021 na tarehe 28 Juni 2021 utakabidhiwa katika Mkoa wa Simiyu.
Kauli mbiu ya mbio maalum za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu “TEHAMA ni Msingi wa Taifa Endelevu: Itumike kwa Usahihi na Uwajibikaji.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa